Ni mambo gani yanayomfanya mtu kumuogopa Allaah na kumkurubia?

Swali: Ni mambo gani ambayo yanapelekea mtu kumuogopa Allaah, kujua kuwa anamuona, kutarajia thawabu zilizoko Kwake na kumpenda ili mja aweze kufanya yale Allaah aliyomwamrisha na kujiepusha na yale Aliyomkataza?

Jibu: Kusoma Qur-aan kwa wingi kwa kuizingatia na kuifikiria. Vilevile mtu anatakiwa kutazama alama za Allaah kubwa kama vile mbingu, ardhi, jua, mwezi na nyota. Vilevile mtu anatakiwa kutazama alama za Allaah kubwa kama vile kunyesha kwa mvua, kutonyesha kwake n.k. Pia mtu anatakiwa kutazama neema za Allaah. Kwa sababu yule atakayetazama alama za Allaah atampenda Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hii imekuja katika Athar:

“Mpendeni Allaah kutokana na neema anazokupeni.”

Maumbile ya mtu ni kuwa anampenda yule anayemtendea wema. Hakuna yeyote ambaye ana wema mkubwa na neema nyingi kuliko Allaah (´Azza wa Jall). Isitoshe anatakiwa kupupia kuuhudhurisha moyo katika swalah. Kwa sababu hili ni miongoni mwa sababu za kuufanya moyo kuwa na unyenyekevu. Pia zingatia maneno ya Allaah (Ta´ala):

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao ni wenye kunyenyekea.”[1]

Hizi ni Aayah za mwanzoni. Katika Aayah za mwishomwisho imekuja:

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ

“Ambao wanazihifadhi swalah zao.”[2]

Zingatia kuwa swalah imeambatana na matendo yote na sifa zote za kheri. Kwa hivyo ni lazima kwako kushikamana na swalah na kuwa na unyenyekevu ndani yake. Kwani hakika swalah inazuia kutokamana na machafu na maovu:

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ

“Takeni msaada kupitia subira na swalah.”[3]

[1] 23:01-02

[2] 23:09

[3] 02:45

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthyamiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (40) http://binothaimeen.net/content/904
  • Imechapishwa: 13/07/2020