Swali: Ni nini maana ya:

“Anayekaribia kwangu shibri moja, Namkaribia dhiraa moja. Anayenijia akitembea, Namjia kwa kuchapuka”?

Jibu: Hii ni Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

“Mimi niko vile mja Wangu anavyonidhania. Mimi niko pamoja naye pale anaponiomba. Akinitaja moyoni mwake, basi Nitamtaja katika nafsi Yangu. Akinitaja katika mkusanyiko, Nitamtaja katika mkusanyiko ulio bora kuliko huo. Akinikaribia shibiri moja, basi Mimi namkaribia dhiraa moja. Akinikaribia dhiraa moja, basi Mimi namkaribia pima. Akinijia kwa kutembea, basi Mimi namwendea kwa kuchapuka.” [1]

Hii ni kutoka kwa Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) kuwahamasisha waja Wake kumtaja na kuharakisha katika kumtii (Subhaanahu wa Ta´ala).

Tafsiri yake inarejea Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna ajuaye namna ya ukaribu huu kutoka Kwake isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Kama tunavyosema kuhusu kulingana Kwake juu ya ‘Arshi, kushuka Kwake, ghadhabu Yake na rehema Yake; sifa zote hizi zinalingana Naye, hazifanani na za viumbe na wala namna yake haijulikani isipokuwa Kwake.

Kwa hiyo hatubainishi namna ya ukaribu Wake, kuja Kwake, kutembea Kwake na kuchapuka Kwake. Bali tunasema: ni kwa namna inayomfaa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini miongoni mwa matunda yake na maana yake ni kwamba Yeye ni mwepesi zaidi wa kuleta kheri kwetu na ni mwenye rehema zaidi kwetu (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] al-Bukhaariy (7405) na Muslim (2675).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3403/معنى-حديث-من-تقرب-مني-شبرا
  • Imechapishwa: 07/09/2026