Zirr bin Hubaysh (Rahimahu Allaah) alimuuliza Swafwaan bin ´Assaal (Radhiya Allaahu ´anh) kuhusiana na kupangusa juu ya soksi na kama ana lolote kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo ambapo akawa ameitikia “Ndio.” Alikuwa akituamrisha tunapokuwa safarini au wasafiri basi tusivue soksi zetu isipokuwa ikiwa kama tuko na janaba. Lakini tufanye hivo [kupangusa juu yake] wakati wa haja kubwa, ndogo na kulala.

Hadiyth hii kuna dalili juu ya kuthibiti kupangusa juu ya soksi. Kumepokelewa Hadiyth nyingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo. Wanachuoni wametendea hilo kazi. Baadhi ya wanachuoni, wale ambao wameandika vitabu vya ´Aqiydah, wamefikia mpaka kuingiza ndani yake suala la kupangusa juu ya soksi kwenye vitabu vya ´Aqiydah. Hilo ni kwa sababu Raafidhwah wameenda kinyume na hilo. Hawakuthibitisha suala la kupangusa juu ya soksi bali kinyume chake wamelikanusha.

Lililo la ajabu ni kwamba miongoni mwa waliopokea kupangusa juu ya soksi ni pamoja na ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh). Pamoja na hivyo wao wanalipinga na hawalitendei kazi. Hivyo ikawa jambo la kupangusa kwenye soksi ni katika alama za Ahl-us-Sunnah na ni miongoni mwa mambo yaliyopokelewa kwa mapokezi mengi kwao kiasi cha kwamba hawana shaka yoyote juu ya kuthibiti hilo kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imaam Ahmad amesema:

“Sina shaka yoyote ndani ya moyo wangu kuhusu kupangusa juu ya soksi. Ni jambo lina Hadiyth arobaini kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/110-111)
  • Imechapishwa: 08/02/2023