36. Dalili kuthibitisha kuwa utegemezi ni ´ibaadah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya utegemeaji ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَعَلَى اللَّـهِ فَتَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Na kwa Allaah pekee tegemeeni ikiwa nyinyi ni waumini!”[1]

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Na yeyote yule atakayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.”[2]

MAELEZO

Utegemezi ni kule kumtegemea Allaah katika kupata matokeo baada ya kufanya sababu. Kwa hivyo tegemeo la moyo wako kupata matokeo anafanyiwa Allaah pekee. Unafanya sababu ambazo Allaah amekuamrisha kufanya ikiwa ni pamoja na kutafuta riziki na mkononi mwako uwe na taaluma unayochuma kwayo, kwa msemo mwingine unafanya sababu kisha unamtegemea Allaah kupata matokeo, matunda na faida.

 Maneno Yake (Ta´ala):

وَعَلَى اللَّـهِ

“Na kwa Allaah pekee… “

Bi maana si kwa mwingine. Hili linafidisha ukomo na kufupika. Kwa sababu miongoni mwa mifumo inayotumika kwa watu wa balagha ni kwamba kumetangulizwa kitu ambacho kilitakiwa kicheleweshwe. Msingi wake ni ilitakiwa iwe:

توكلوا على الله

“Mtegemeeni Allaah… “

Isitoshe katika Aayah hiyo kuna amri inayoonyesha ulazima wa kutegemea Allaah (Jalla wa ´Alaa) na mtu ayaegemeze mambo yake Kwake. Kwa hivyo Aayah imefahamisha ulazima wa kutegemea na kwamba ni katika ´ibaadah.

Maneno Yake (Ta´ala):

إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“… ikiwa nyinyi ni waumini!”

Bi maana ikiwa kweli mnamwamini Allaah (Jalla wa ´Alaa) basi Yeye pekee mtegemeeni. Amefanya kumtegemea Allaah ni sharti katika imani. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hapa kuna dalili inayoonyesha kukanushwa imani wakati wa kunakosekana utegemezi. Asiyekuwa na utegemezi basi hana imani.”[3]

Maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Na yeyote yule atakayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.”

Yule ambaye anatoshelezwa na Allaah basi hakuna mwingine anayemuhitaji.

[1] 05:23

[2] 65:03

[3] Madaarij-us-Saalikiyn (02/128).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 08/02/2023