Fadhilah za kusimama usiku mzima ni ndani ya Ramadhaan peke yake?

Swali: Kuna Hadiyth yenye maana isemayo:

“Hakika yule atakayesimama pamoja na imamu mpaka akaondoka, basi ataandikiwa ameswali usiku mzima.“

Je, hilo linahusu Ramadhaan peke yake au miezi mingine pia?

Jibu: Ni pale anaposwali nyuma ya imamu katika Ramadhaan. Kwa sababu hilo limepokelewa ndani ya Ramadhaan. Basi mtu huyo Allaah atamwandikia kuwa amesimama usiku mzima. Akiswali pamoja naye mpaka akaondoka basi ataandikiwa kuwa ameswali usiku mzima. Hapa kuna kuhamasisha swalah ya mkusanyiko, kuhimiza swalah ya mkusanyiko kama vile swalah ya Tarawiyh na kuswali kisimamo cha usiku katika kumi la mwisho pamoja na imamu.

Kuhusu nyusiku zingine sijui kinachofahamisha jambo hilo. Lakini kwa ambaye baadhi ya nyusiku ataswali mkusanyiko na ndugu yake na mmoja akawaswalisha wengine, basi kunatarajiwa juu yao kheri kubwa. Kufanya hivo kuna kushirikiana katika wema na kumcha Allaah. Kuna matarajio Hadiyth ikawakusanya kama ambao wamefanya hivo katika Ramadhaan.

Ama kuhusu swalah ya faradhi ya ´Ishaa kuna dalili yake:

“Ambaye ataswali ´Ishaa katika mkusanyiko, basi ni kama ambaye ameswali nusu ya usiku. Na ambaye ataswali ´Ishaa na Fajr kwa mkusanyiko, basi ni kama ambaye amesimama usiku.”

Hili ni kuhusu fadhilah ya mkusanyiko licha ya kwamba ni wajibu. Swalah ya mkusanyiko ni lazima na ndani yake kuna fadhilah kubwa pia.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/10225/هل-يختص-رمضان-بفضل-القيام-مع-الامام-حتى-ينصرف
  • Imechapishwa: 06/04/2023