Faatwimah bint Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)

Alikuwa ndiye bibi wa wanawake katika zama zake na sehemu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa ni Umm Abiyhaa[1], msichana wa bwana wa viumbe, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Abul-Qaasim Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim bin ´Abdil-Manaaf al-Qurashiyyah al-Haashimiyyah.

Alizaliwa punde kdiogo kabla ya utume na akaolewa na ´Aliy bin Abiy Twaalib katika mwezi wa Dhul-Hijjah, au kidogo kabla ya hapo, mwaka wa 02 baada ya vita vya Badr.

Ibn-ul-Barr amesema:

”Alimwingilia baada ya vita vya Uhud. Akamzalia al-Hasan, al-Husayn, Muhsin, Umm Kulthuum na Zaynab.”

Amepokea kutoka kwa baba yake.

Baadhi ya waliopokea kutoka kwake ni pamoja na mwanae al-Husayn, ´Aaishah, Umm Salamah na Anas bin Maalik. Mapokezi yake yako katika vile vitabu Sita.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda, akimkirimu na akifurahishwa naye. Anazo fadhilah nyingi tukufu. Alikuwa ni mwenye subira, mwenye dini, mwema, mwenye kujihifadhi, mwenye kinaa na mwenye kumshukuru Allaah.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alighadhibika kwa ajili yake wakati alipofikiwa na khabari kwamba Abul-Hasan anataka kumposa msichana wa Abu Jahl, jambo ambalo alikuwa anaona kuwa linafaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

”Naapa kwa Allaah hatokusanyika msichana wa Mtume wa Allaah pamoja na msichana wa adui wa Allaah. Si vyenginevyo Faatwimah ni kipande kutoka kwangu. Kinanitesa kile kinachomtesa na kinaniudhi mimi kile kinachomuudhi yeye.”

Baada ya hapo ´Aliy akaacha kumposa kwa ajili ya kumzingatia Faatwimah. Hakuoa juu yake wala kuchukua mjakazi yeyote kipindi cha uhai wake. Baada ya kufariki kwake ndipo akaoa na kufanya wajakazi – Allaah awawie radhi.

Wakati alipofariki Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Faatwimah akamwambia Anas bin Maalik:

”Ee Anas! Ni vipi mtaweza kumakinisha kumwagilia udongo juu ya Mtume wa Allaah?”[2]

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia yeye alipokuwa anataka kukata roho:

”Mimi nitafariki kutokana na maradhi haya.”

Akaanza kulia. Akamweleza kuwa yeye ndiye atakuwa wa kwanza katika familia yake kuungana naye na kwamba yeye ni bibi wa wanawake wa Ummah huu. Akacheka na hakumweleza yeyote aliyomwambia. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofariki, ´Aaishah akamuuliza juu ya hilo na ndipo alimweleza siri aliyompa[3].

Wakati alipofariki baba yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Faatwimah akawa na matumaini ya kumrithi baba yake. Akamwendea Abu Bakr as-Swiddiyq na kumwomba kitu hicho. Ndipo akamweleza kwamba yeye amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Sisi [Mitume] haturithiwi. Kile tunachoacha ni swadaqah.”[4]

Akachukulia vibaya lakini baadaye akaacha kujishughulisha nacho.

Alikufa takriban miezi mitano baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aliishi miaka 24 au 25. Miaka mingi iliotajwa ni kwamba aliishi miaka 29. Hata hivyo maoni ya kwanza ndio sahihi zaidi.

Alikuwa mdogo kuliko Zaynab, mke wa Abul-´Aasw bin ar-Rabiy´, Ruqayyah, mke wa ´Uthmaan bin ´Affaan. Kizazi cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kilikatika kutoka pande zote isipokuwa kutokea kwa Faatwimah.

az-Zubayr bin Bakkaar amesema:

”Kizazi cha Zaynab kilitokomea.”

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtazama ´Aliy, Faatwimah, al-Hasan na al-Husayn akasema: ”Mimi ni mwenye kumpiga vita yule mwenye kuwapiga vita na mwenye kumpa amani yule mwenye kuwapa amani.”[5]

Abu Sa´iyd al-Khudriy ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna yeyote anayetuchukia sisi Ahl-ul-Bayt isipokuwa Allaah atamwingiza Motoni.”[6]

Hudhayfah ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Malaika aliteremka na akanipa bishara njema ya kwamba Faatwimah ni bibi wa wanawake wa Peponi.”[7]

Ibn ´Abaas ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanawake bora wa Peponi ni Khadiyjah na Faatwimah.”[8]

Wasichana aliozaa ni Umm Kulthuum, mke wa ´Umar bin al-Khattwaab, na Zaynab, mke wa ´Abdullaah bin Ja´far bin Abiy Twaalib.

 Ibn ´Abaas ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanawake bora wa Peponi ni Khadiyjah bint Khuwaylid, Faatwimah bint Muhammad, Maryam na ´Aasiyah.”

´Aaishah amesema:

“Faatwimah aliishi miezi misita baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akazikwa usiku.”[9]

Abu Ja´far al-Baaqir amesema:

”Alikuwa na miaka 28 wakati alipofariki. Alizaliwa wakati ilipojengwa Ka´bah.”

Amesema tena:

“Alioshwa na ´Aliy.”

[1] Katika ”al-Iswaabah” (13/71) na ”Usd-ud-Ghaabah” (07/25) imekuja kwamba kun-yah yake ilikuwa Umm Abiyhaa (Mama yake baba yake).

[2] al-Bukhaariy (8/113).

[3] al-Bukhaariy (6/462).

[4] al-Bukhaariy (6/139).

[5] Ahmad (2/442).

[6] al-Haakim (3/150) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[7] al-Haakim (3/151) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[8] Ahmad (1/293) na al-Haakim (02/594) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[9]  al-Haakim (3/162).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (2/118-134)
  • Imechapishwa: 07/01/2021