86. Tafsiri inayobainisha maana ya shahaadah ya kwanza II

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ ۚ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ

“Sema: “Enyi watu wa Kitabu! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu – kwamba tusiabudu yeyote isipokuwa Allaah Pekee wala tusimshirikishe Yeye na chochote wala wasiwafanye baadhi yetu wengine kuwa ni waungu badala ya Allaah.” Wakikengeuka; basi semeni: “Shuhudieni kwamba sisi ni waislamu.”[1]

MAELEZO

Sema… – Aayah hii ni kutoka katika Suurah “Aal ´Imraan” ambayo imeteremka juu ya mjumbe wa kinaswara wa Najraan ambaye alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akajadiliana naye na akamuuliza. Kulitokea maneno marefu kati yao wawili. Ni manaswara wa kiarabu. Mwishoni Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaomba wafanyiane laana:

فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنفُسَنَا وَأَنفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَل لَّعْنَتَ اللَّـهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ

“Sema: “Njooni tuwaite wana wetu na wana wenu na wanawake wetu na wanawake wenu na nafsi zetu wenyewe na nafsi zenu, kisha tuombe Mubaahalah, tuifanye laana ya Allaah iwe juu ya waongo.”[2]

Wakati alipowaomba jambo hilo wakaogopa na hakuwaapiza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Matokeo yake wakawa wanamlipa kodi. Kwa sababu walijua kuwa wamo katika batili na kwamba yeye ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walikuwa wanajua kuwa wao ndio waongo. Lau wangeliombeana laana basi wangeliteremkiwa na moto na wakachomeka papo hapo. Wakakataa na wakasema kuwa badala yake watalipa kodi ambapo Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakubali kodi kutoka kwao. Imebainika kuwa Allaah amemwamrisha kwa yale yaliyomo ndani ya Aayah hii.

Katika Aayah hii kuna maana ya shahaadah. Maneno Yake:

أَلَّا نَعْبُدَ

“… tusiabudu.. “

Huku ni kukanusha.

إِلَّا اللَّـهَ

“… isipokuwa Allaah. pekee.“

Huku ni kuthibitisha. Huu ndio uadilifu ambao mbingu na ardhi zimesimama kwao. Mbingu na ardhi imesimama kwa Tawhiyd na uadilifu. Hatumshirikishi katika ´ibaadah Yake si al-Masiyh ambaye mnadai kuwa ndiye mungu na mnamwabudu badala ya Allaah, Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), yeyote katika Mitume, waja wema wala yeyote katika mawalii:

 أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ

“… tusiabudu yeyote isipokuwa Allaah Pekee wala tusimshirikishe Yeye na chochote wala wasiwafanye baadhi yetu wengine kuwa ni waungu badala ya Allaah.”

 Kama ambavo nyinyi mlivowafanya watawa na marabi wenu waungu badala ya Allaah (Ta´ala):

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا

“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah na al-Masiyh, mwana wa Maryam, ilihali hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Mungu Mmoja pekee.”[3]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha maana ya kuwafanya watawa na marabi waungu badala ya Allaah kwamba maana yake ni kule kuwatii katika kuhalalisha yale aliyoharamisha Allaah na kuharamisha yale aliyohalalisha Allaah[4]. Hiyo ndio maana ya kuwafanya waungu badala ya Allaah. Hapo ni pale wanapohalalisha yale aliyoharamisha Allaah na wanaharamisha yale aliyohalalisha Allaah. Wakiwatii katika hayo wanakuwa wamewafanya ni waungu. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pekee ndiye mwenye kuwawekea watu Shari´ah, mwenye kuhalalisha na mwenye kuharamisha.

فَإِن تَوَلَّوْا

“Wakikengeuka.”

Wasikubali wito wa Tawhiyd.

فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ

“Basi semeni: “Shuhudieni kwamba sisi ni waislamu.”

Shuhudieni kuwa sisi ni wenye kumwabudu Allaah peke yake na kwamba nyinyi ni makafiri. Wabainishieni upotevu wa yale waliyomo.

Ndani ya Aayah hii kuna kujitenga mbali na dini ya washirikina na kuwa muwazi juu ya jambo hilo. Shuhudieni kwamba sisi ni waislamu. Ndani ya haya kuna ulazima wa kutangaza ubatilifu wa yale waliyomo washirikina, kutonyamazia jambo hilo, kutangaza ubatilifu wa shirki na kuwaraddi watu wake.

Kwa kufupiza ni kwamba shahaadah ina nguzo mbili; kukanusha na kuthibitisha. Unapoulizwa ni zipi nguzo za ”Laa ilaaha illa Allaah” unajibu kwamba ni kukanusha na kuthibitisha.

[1] 03:64

[2] 03:61

[3] 09:31

[4] Tazama Hadiyth ya ´Adiyy bin Haatim (Radhiya Allaahu ´anh) iliopokelewa na at-Tirmidiy (3095) ambapo ndani yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Wao hawakuwa wakiwaabudu. Lakini walikuwa wakiwahalalishia kitu basi nao wanakihalalisha na wanapowaharamishia kitu nao wanakiharamisha.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 169-173
  • Imechapishwa: 12/01/2021