Swali: Kuna wenye kusema ni wajibu kwa mtu kuepuka kuzungumzia Bid´ah na Sunnah. Mwalimu akizungumzia juu ya mambo haya anatumbukia katika matatizo na watu wengine kwa sababu watu wengi ni wazushi na hawajui ni nini Sunnah. Kwa ajili hiyo mtu anatumbukia katika migogoro pamoja nao. Hivyo fitina inazuka kwa vile watu hawayakubali mafunzo haya kwa kuzingatia ya kwamba yanaenda kinyume na matamanio yao. Je, mwenye kusahihisha ´Aqiydah kwa kuisafisha na Bid´ah anaitwa “mfitinishaji” au yule mwenye kwenda kinyume na maamrisho ya Allaah ndiye ambaye anasababisha fitina?

Jibu: Mlinganizi anatakiwa kuwa mjuzi juu ya yale anayolingania na yale anayokataza, mwenye hekima juu ya yale anayoamrisha na yale anayokataza. Vilevile anatakiwa kupima kati ya manufaa; atangulize yale yenye manufaa zaidi juu ya yale yasiyokuwa na manufaa sana. Sambamba na hilo aangalie madhara na kutanguliza yale yenye madhara kidogo ili kuepuka makubwa zaidi. Manufaa na madhara yote mawili yakikutana na manufaa yakawa na nguvu zaidi ayatendee kazi. Na madhara yakiwa ndio ambayo yana nguvu basi asifanye kitu.

Kujengea juu ya hilo anatakiwa kuithibitisha Sunnah na kuibainisha na akemee Bid´ah na kuwabainishia nayo watu. Lakini hata hivyo anatakiwa kufanya hayo kwa hekima, maneno mazuri na kuzungumza kwa njia ilio nzuri. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala) katika Qur-aan:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ

“Waite [watu] katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.” (16:125)

Kwa kufanya hivyo hatoitwa kuwa ni mfitinishaji.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (2/336-337)
  • Imechapishwa: 23/08/2020