Swali: Ni ipi hukumu ya kusoma Qur-aan kwa pamoja? Ninaomba mnitajie dalili kutoka kwenye Qur-aan au Sunnah.

Jibu: Kusoma Qur-aan ni ´ibaadah na ni miongoni mwa mambo bora kabisa ambayo mtu anajikurubisha kwayo kwa Allaah (Ta´ala). Msingi katika utekelezaji wa ´ibaadah ni iwe katika sifa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakifanya. Haikuthibiti kutoka kwake yeye wala Maswahabah zake ya kwamba walikuwa wakisoma kwa pamoja kwa sauti moja. Bali kila mmoja alikuwa anasoma kivyake au mmoja anasoma na wengine huku wanasikiliza. Imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu.”

“Atakayeuzusha katika dini yetu yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Atakayefanya kitendo ksichokuwemo katika dini yetu atarudishiwa mwenyewe.”

Vilevile imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alimuamrisha ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amsomee Qur-aan ambapo akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nikusomee ilihali imeteremshwa kwako?” Akasema:

“Hakika mimi napenda kuisikia kutoka kwa mwengine.”

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (112-113/04)
  • Imechapishwa: 22/08/2020