Acha kazi ya haramu utaruzukiwa na Allaah

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ

“Na yeyote yuleanayemcha Allaah, atamjaalia njia [ya kutoka katika matatizo] na atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii.” (65:02-03)

Hii pia ni faida kubwa. Allaah atakuruzuku kwa njia usiyoitegemea.

Tuchukulie kuna mtu anachuma mali kwa njia ya haramu kama kufanya ghushi, ribaa na nyenginezo. Akanasihiwa juu ya hili na akaacha kwa ajili ya Allaah, basi Allaah atamjaalia njia ya kutokea na kumruzuku kwa njia asiyoitegemea. Lakini pamoja na hivyo usiwe na haraka. Usifikirie kuwa faraja ikichelewa haitokuwa. Allaah anaweza kumjaribu mja na kumcheleweshea thawabu ili kumpima na kuona kama atarudi katika ile dhambi au hatorudi.

Kwa mfano unafanya kazi ya ribaa na kukawa mtu akakupa mawaidha na ukaacha hilo. Ukakaa mwezi mmoja mpaka miwili na usione faida yoyote, usivunjike moyo na kusema iko wapi riziki hiyo iliyosemwa. Kuwa na subira. Amini na usadikishe ahadi ya Allaah na utaipata. Usiwe na haraka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu hujibiwa pindi anapoomba midhali hatokuwa na haraka.” Wakasema: “Ni vipi atakuwa na haraka, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Husema “Nimeomba na sikuitikiwa.”[1]

Kuwa ni mwenye subira. Acha aliyokuharamishia Allaah na usubiri faraja. Riziki utaipata kwa njia usiyoitegemea.

[1] al-Bukhaariy (6340) na Muslim (2735).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/517-518)
  • Imechapishwa: 26/06/2023