Nimekwishataja namna ambavyo kuna watu wanaotofautiana na sisi kuhusiana na kuyaingiza matendo katika imani. Ijapo ni wenye kutofautiana nasi, wameenda katika madhehebu ambayo kunaweza kutokea makosa katika mfano wake. Kisha baadaye kukazuka kundi la tatu ambalo limepinda kutokamana na makundi yote mawili. Hawana lolote kuhusiana na wanazuoni na dini. Kwa mujibu wao imani ni kule kutambua kwa moyo peke yake hata kama hakuna maneno wala matendo. Kwa mujibu wetu tunaona kuwa kauli hii inatoka nje ya dini takasifu kwa sababu ya kupingana kwake na maneno ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa sababu inarudisha na kuyakadhibisha. Hukumsikia Allaah akisema:

قُولُوا آمَنَّا بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنزِلَ إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَا أُوتِيَ النَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُون

”Semeni: “Tumemwamini Allaah na yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl na Ishaaq na Ya’quub na al-Asbaatw na aliyopewa Muusa na ‘Iysaa na waliyopewa Manabii kutoka kwa Mola wao, hatutofautishi baina ya mmoja yeyote miongoni mwao nasi Kwake tunajisalimisha.”[1]?

Amefanya maneno ni faradhi kama ambavo amefanya utambuzi ni faradhi. Hakuridhia tu kule kutambua kwetu kwa mioyo yetu.

Kisha akatuwajibishia na kutufaradhishia kutambua na kuamini vitabu na Mitume. Hakumfanya yeyote kuwa mwenye kuamini isipokuwa baada ya kumsadikisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale yote aliyokuja nayo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنزَلَ مِن قَبْلُ ۚ وَمَن يَكْفُرْ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا

“Enyi mlioamini! Mwaminini Allaah na Mtume Wake na Kitabu alichokiteremsha kwa Mtume Wake na Kitabu alichokiteremsha kabla. Na atakayemkufuru Allaah na Malaika Wake na Vitabu Vyake na Mitume Yake na siku ya Mwisho, basi kwa hakika amepotoka upotofu wa mbali.”[2]

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.”[3]

يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ

“Wanatambua kama wanavyowatambua watoto wao.”[4]

Bi maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Licha ya kwamba wanamjua (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Allaah hakuthibitisha imani yao kwa sababu hawakuthibitisha ujumbe wake kwa kutamka. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa kuhusu imani, alijibu kwa kusema:

“Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini makadirio, kheri na shari yake.”[5]

Ipo mifano mingi kama hii isiyodhibitika.

[1] 2:136

[2] 4:136

[3] 4:65

[4] 2:146

[5] Muslim.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 59-61
  • Imechapishwa: 27/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy