Haki iko pamoja na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Imechukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah; ya kwamba imani ni kutamka kwa mdomo, kuamini ndani ya moyo na matendo ya viungo.

Maneno ya mtunzi:

“Inazidi kwa matendo mema.”

Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ

“Na inapoteremshwa Suurah, basi miongoni mwao wako wanaosema: “Nani kati yenu [Suurah] hii imemzidishia imani?” Ama wale walioamini huwazidishia imani nao wanafurahia.”[1]

Ni dalili inayofahamisha kuwa imani inazidi. Wapotevu wanaona kuwa haizidi na kwamba ni kitu kimoja kilichoko ndani ya moyo. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا

“Hakika si vyenginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake basi huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea. Ambao wanasimamisha swalah na hutoa sehemu ya vile Tulivyowaruzuku; – hao ndio waumini wa kweli.”[2]

Ametaja matendo na akayafupiza matendo kwa watu hawa:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ

“Hakika si vyenginevyo waumini… “

Ametaja maneno na ametaja vilevile matendo kama mfano wa kusimamisha swalah, kutoa zakaah na kuogopa kwa mioyo. Hii ndio imani. Ni dalili inayofahamisha kuwa inazidi kwa matendo mema. Imani inazidi kwa swalah, kwa zakaah na kwa kusoma Qur-aan. Imani ni yenye kuzidi. Amesema (Ta´ala):

وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا

“… na iwazidishie imani wale walioamini.”[3]

Ni dalili inayofahamisha kuwa imani inazidi na vivyo hivyo inapungua. Kwa dalili kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu. Ya juu yake ni “Laa ilaaha illa Allaah” na ya chini yake ni kuokota chenye kudhuru kutoka njiani.”[4]

Ni dalili iliyofahamisha kuwa imani ina ya juu yake na ya chini yake. Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule katika nyinyi atakayeona maovu, basi ayazuie kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa mdomo wake. Asipoweza, afanye hivo kwa moyo  wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”

Ni dalili iliyofahamisha kuwa imani inadhoofika na inapungua. Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Mtoeni Motoni yule ambaye moyoni mwake mna imani sawa na uzani wa mbegu ya hardali.”

Ni dalili inayofahamisha kuwa imani inapungua mpaka inakuwa mfano wa mbegu ya hardali. Kwa hiyo watu hawalingani katika imani. Baadhi wana imani yenye nguvu zaidi kuliko wengine.

Murji-ah wanasema kuwa watu wake katika msingi wake wanalingana. Vilevile wanasema kuwa hakuna tofauti kati ya imani ya Abu Bakr na imani ya mtu muovu kabisa katika watu. Wanaona kuwa wote ni waumini.

Kuhusu Ahl-us-Sunnah wanaona kuwa imani ya mtu huyu inalingana na mlima na imani ya huyu mwingine inalingana na mfano wa chembe kidogo ya atomu au mfano wa mbegu ya hardali. Hawalingani kati yao.

Hii ndio maana ya maneno yake:

“Inazidi kwa matendo mema na inapungua kwa maasi.”

Kila ambavo muislamu anavomtii Mola Wake imani yake inazidi na kila ambavyo anamili kumuasi Mola Wake imani yake inashuka. Haya ndio madhehebu ya haki. Hii ndio maana ya imani sahihi.

[1] 09:124

[2] 08:02-04

[3] 74:31

[4] Muslim (35) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 136-137
  • Imechapishwa: 01/06/2021