Kuishi katika nchi za makafiri kwa ajili ya kulingania

Swali: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika mimi najitenga mbali na muislamu anayeishi kati ya washirikina.”

Hii leo tunaona mamia ya waislamu wanaishi kati ya washirikina. Wahisani wameenda huko na kujenga masomo mosi kwa ajili ya kuwafunza waislamu na pili kwa ajili ya kulingania katika Uislamu. Je, inafaa kwa mwalimu kwenda kuishi huko kwa ajili ya kufundisha na kulingania katika Uislamu? Je, inafaa kwake kukubali haya ilihali atakuwa akiishi kati ya washirikina?

Jibu: Hapana shaka kwamba kuna madhara kuishi kati ya washirikina. Mtu anaiweka nafsi yake katika mtihani na shari. Lakini ikiwa mtihani na shari hii inapelekea katika kheri kubwa, kwa mfano akaenda huko kuwalingania watu katika Uislamu au kuwafunza waislamu ´Aqiydah sahihi, basi kufanya hivo hakuna neno. Kwa sababu katika hali hiyo manufaa ni makubwa zaidi kuliko madhara yanayochelewa.

Pamoja na kwamba Hadiyth hiyo inaweza kufasiriwa kwamba inamuhusu yule ambaye hawezi kuidhihirisha dini yake tofauti na yule ambaye anaweza kuidhihirisha dini yake. Hata hivyo bora ni kuifahamu kwa ujumla. Katika hali hiyo itakuwa inafaa kwake kuishi huko ikiwa kuishi kwake huko kuna manufaa zaidi juu ya Uislamu na kwa waislamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (57 A)
  • Imechapishwa: 01/06/2021