98. Wanamme ndio wanaomshusha maiti ndani ya kaburi na jamaa zake ndio wenye kutangulizwa

96- Mwanaume pasi na mwanamke ndiye atasimamia jambo la kumshusha maiti ndani ya kaburi hata kama maiti ni wa kike. Hilo ni kutokana na mambo yafuatayo:

1- Ndio jambo lililozoeleka katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ndivo kitendo za waislamu kilivopita mpaka hii leo. Kumepokelewa juu yake Hadiyth ya Anas katika masuala ya 99.

2- Wanamme ndio wenye nguvu zaidi kwa jambo hilo.

3- Lau hilo lingesimamiwa na wanawake basi lingepelekea kuonekana kitu katika miili yao mbele ya wanaume wa kando, jambo ambalo halijuzu.

97- Jamaa zake maiti ndio wenye haki zaidi ya kumteremsha. Hilo ni kutokana na kuenea kwa maneno Yake (Ta´ala):

وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ

“Jamaa wa nasaba[1] wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika Shari´ah ya Allaah.”[2]

Pia ni kutokana na Hadiyth ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

“Nilimuosha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nikaenda kuona yale yanayomtokea maiti ambapo sikuona chochote. Alikuwa mzuri katika hali ya kuwa hai na baada ya kufa. Watu wanne ndio walisimamia kumzika na kumsitiri pasi na wengine: ´Aliy, al-´Abbaas, al-Fadhwl na Swaalih[3] ambaye ni mtumwa aliyeachwa huru na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye akachimba Lahd kwa ajili ya Mtume wa Allaah na akaziba juu yake kwa matofali.”

Ameipokea al-Haakim (01/362) na al-Bayhaqiy (04/53) kutoka kwake kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. al-Haakim ameisahihisha kwa sharti za al-Bukhaariy na Muslim na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

Ina shawahidi kutoka katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas ambayo tumetangulia kuitaja katika masuala uya 94, uk. 144-145.

Shahidi nyingine kutoka kwa Sha´biy ambayo ina cheni ya wapokezi isiyokuwa na Swahabah. Lakini hakumtaja Swaalih ambaye ni mwacha huru wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ameipokea Abu Daawuud (02/69) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwake.

Kwake yeye amepokea kutoka kwa Marhab – ambaye ni Ibn Abiy Marhab:

“Kwamba wao (bi maana ´Aliy, al-Fadhwl na ndugu yake) walimwingiza ´Abdur-Rahmaan  bin ´Awf pamoja nao. Wakati ´Aliy alipomaliza akasema: “Wanaomsimamia mtu ni wale jamaa zake.”

Marhab au Ibn Abiy Marhab wanachuoni wametofautiana juu ya uswahabah wake[4].

Kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Abzaa amesema:

“Niliswali pamoja na ´Umar bin al-Khattwaab kumswalia Zaynab bint Jahsh katika mji wa al-Madiynah. Akapiga Takbiyr nne kisha akatuma ujumbe kwa wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Wanapendekeza nani amwingize ndani ya kaburi?” Msimulia wa Hadiyth anasema: “Ilikuwa inampendeza yeye ndiye asimamie jambo hilo.” Wakamrudishia ujumbe wenye kusema: “Tazama wale waliokuwa wakimuona katika hali ya uhai wake na hao ndio wamwingize ndani ya kaburi. ´Umar akasema: “Mmesema kweli.”

Ameipokea at-Twahaawiy (03/304-305), Ibn Sa´d (08/111-112) na al-Bayhaqiy (03/53) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[1] Ni baba, wazazi wake baba, mtoto, mtoto na watoto wake, kisha wale ndugu kwa baba na mama mmoja, kisha wale ndugu upande wa baba, kisha watoto wao, kisha wale maami wa baba na wa mama na watoto wao. Kisha kila ambaye ni ana ujamaa wa karibu. Hivo ndivo ilivyotajwa katika ”al-Muhallaa” (05/143) na mfano wake katika ”al-Majmuu´” (05/290).

[2] 08:75

[3] Laqabu yake ni Shuqraan. Tazama ”Nuzhat-ul-Albaab” (1684) na tamko ni la Ibn Hajar.

[4] Hadihth hiyo na ile ilioko kabla yake ni katika Mursal za Sha´biy. Ni ushahidi wenye nguvu kabisa juu ya Hadiyth ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 186-187
  • Imechapishwa: 03/03/2022