98- Inajuzu kwa mume kusimamia zoezi la mazishi ya mke wake. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwangu katika ile siku ambayo maradhi yameanza ambapo nikasema: “Ee kichwa changu!” Akasema: “Nimetamani yakutokee kipindi ambacho ni hai ambapo nikakuandaa na nikakuzika.” ´Aaishah akasema: “Nikasema hali ya kuwa na wivu “Kana kwamba mimi kwako wewe siku hiyo nilikuwa biharusi ukilinganisha na baadhi ya wako zako.” Akasema: “Ee na mimi kcihwa changu!” Niitikie baba yako na ndugu yako ili nipate kumwandikia Abu Bakr kitabu. Kwani hakika mimi nachelea asije kusema msemaji na akatamani mwenye kutamani: “Kwamba mimi ndiye mstahiki zaidi. Lakini Allaah (´Azza wa Jall) na waumini hawamtaki mwingine isipokuwa Abu Bakr.”

Ameipokea Ahmad (06/144) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Iko katika “Swahiyh-ul-Bukhaariy” mfano wake (10/101, 102), Muslim (07/110) kwa mukhtasari. Inayo njia nyingine kutoka kwa ´Aaishah iliyotangulia katika ukurasa wa 50.

Shaafi´iyyah wameonelea kufaa mume kumzika mke wake. Bali wamesema kuwa yeye ndiye mwenye haki zaidi ya jambo hilo katika jamaa zake ambao tumewataja. Ibn Hazm ameonelea kinyume na hivo ambapo yeye ameonelea kuwa mume anakuja baada yao katika kustahiki. Pengine ndio lililo karibu zaidi na haki kutokana yaliyotangulia ya kuenea kwa Aayah.

99- Lakini hilo limewekewa sharti ikiwa hakufanya jimaa usiku huo. Venginevyo haitokuwa ni jambo lililowekwa katika Shari´ah kwa yeye kumzika. Badala yake mwengine ndiye atakuwa na haki zaidi ya kumzika – ijapo ni mtu wa kando naye – kwa sharti iliyotajwa. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Tulishuhudia maziko ya msichana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na huku Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekaa juu ya kaburi. Tahamaki nikaona macho yake yanatokwa na machozi. Kisha akasema: “Je, yupo miongoni mwenu mtu ambaye hakumjamii usiku [mke wake]?” Abu Twalhah akasema: “Ndio, mimi ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Basi shuka ndani ya kaburi lake [na hivyo akamzika].”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mtume wa Allaah wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema pindi Ruqayyah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alipokufa: “Asiingie ndani ya kaburi mtu ambaye [usiku] amemwingilia mke wake. Hivyo ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) hakuingia kaburini.”

Upokezi wa kwanza ameupokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake (03/122,162), at-Twahaawiy katika “al-Mushkil” (03/304), al-Haakim (04/47), al-Bayhaqiy (04/53), Ahmad (03/126, 228) na mtiririko ni wake na kwake yeye ndio kuna ziada ya pili katika upokezi wake yeye, na kwa at-Twahaawiy na al-Haakim kunayo ziada ya mwanzo na ziada ya mwisho ipo kwa al-Bukhaariy.

Ahmad (03/229-280) amepokea upokezi wa pili, at-Twahaawiy (03/202), al-Haakim (04/47), Ibn Hazm (05/145) kupitia njia nyingine kwa Anas. Mtiririko ni wa Ahmad na ziada ni ya al-Haakim ambaye amesema:

“Hadiyth ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim.”

Mambo ni kama alivosema. adh-Dhahabiy amemkubalia. Isipokuwa baadhi ya maimamu wamempinga jambo la kumwita msichana huyo “Ruqayyah”. al-Bukhaariy amesema katika “at-Tariykh al-Awsatw”:

“Sijui ni kitu gani hichi? Kwani Ruqayyah alifariki na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa Badr na hivyo hakumshuhudia Ruqayyah.”

al-Haafidhw katika “al-Fath” ameipa nguvu kwamba kosa limetokea kwa Hammaad bin Salamah na kwamba msichana huyo alikuwa ni Umm Kulthuum mkewe wa ´Uthmaan. Rejea huko. Hayo ndio maoni ambayo at-Twahaawiy ameyakata katika “al-Mushkil” na akasema:

“Kufa kwake kulikuwa katika mwaka wa tisa baada ya kuhajiri.”

an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´” (05/289):

“Hadiyth hii ni katika Hadiyth ambazo zinajengewa hoja kwamba wanamme ndio wanaosimamia zoezi la maziko ijapo atakuwa ni mwanamke. Ni jambo linalotambulika kuwa Abu Twalhah (Radhiya Allaahu ´anh) ni mtu wa kando kwa wasichana zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini hata hivyo yeye ndiye ambaye alikuwa miongoni mwa wale wanaofaa katika waliohudhuria. Hakukuweko mwanamme ambaye ni Mahram isipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Pengine yeye alikuwa na udhuru wa kushuka ndani ya kaburi lake na vivyo hivyo mume wake. Ni jambo linalojulikana kwamba huyo alikuwa ni dada yake Faatwimah na wengineo katika wale Mahram zake na wengineo waliokuwa huko. Kwa hivyo ikajulisha kuwa hapana nafasi na haifai kwa wanawake kuingia ndani ya kaburi na kuzika.”

al-Haafidhw amesema katika “al-Fath”:

“Katika Hadiyth kuna dalili ya kumpa kipaumbele yule mtu wa mbali kutokamana na kutamani katika jambo la kumleta yule maiti hata kama atakuwa ni mwanamke juu ya baba na mke. Imesemekana pia kwamba alimpa kipaumbele jambo hilo kwa sababu ndio alikuwa mairi zaidi wa jambo hilo, ijapo ni maoni yanayotakiwa kutazamwa vyema. Udhahiri wa mtiririko ni kwamba alimchagua kufanya kazi hiyo kwa sababu usiku huo hakufanya jimaa.”

Hadiyth iko wazi juu ya yale ambayo tumekwishayatolea maelezo. Hayo pia ndio maoni ya Ibn Hazm (Rahimahu Allaah) (05/144-145).

Miongoni mwa mambo ya kushangaza ni kwamba vitabu vyote vya Fiqh ambavo nimesoma au nimevirejea juu ya mada hii ni kwamba hawajadhihirisha masuala haya; si kwa kuyathibitisha wala kuyakanusha. Hii ni dalili miongoni mwa dalili nyingi juu ya hakuna kwa mwanachuoni kujitosheleza kutokamana na vitabu vya Sunnah. Hivo ni kinyume na vile wanavofikiria wale watu wenye ushabiki wa madhehebu kwamba vitabu vya Fiqh vinatosheleza kutokamana na vitabu vya Hadiyth, bali kutokamana na Kitabu cha Allaah – Allaah (Ta´ala) ametakasika kutokamana na yale wanayoyasema madhalimu kutukuka kukubwa. Tazama “Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (01/128-129).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 187-190
  • Imechapishwa: 03/03/2022