17. Umbali wa kwenda mchana na usiku ndio unazingatiwa safari

Swali 17: Tunaomba kuwekewa wazi suala la kufupisha swalah safarini. Je, imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alikamilisha swalah safarini na swalah ya safari inatekelezwa kutegemea na ule umbali na muda? Tunataraji kuwekewa wazi maswali haya pamoja na dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah[1].

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisafiri basi anaswali Dhuhr Rak´ah mbili, ´Aswr Rak´ah mbili na ´Ishaa Rak´ah mbili mpaka pale anaporejea kutoka safarini mwake. Hiki ndicho kilichohifadhiwa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vilevile imepokelewa kutoka kwake ya kwamba alikuwa akiswali kwa kufupisha na kukamilisha. Lakini haikuhifadhiwa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika Hadiyth Swahiyh ya kwamba safarini alikuwa akifupisha mpaka wakati anaporudi. Kuhusu Maghrib alikuwa akiiswali kama ilivyo Rak´ah tatu katika hali ya safari na ya ukazi. Vivyo hivyo Fajr alikuwa akiiswali Rak´ah mbili katika hali ya safari na ya ukazi. Akiswali pamoja nayo Sunnah yake kabla yake katika hali ya safari na ya ukazi ambazo ni Rak´ah mbili nyepesi. Ama Sunnah ya Dhuhr, Sunnah ya ´Aswr, Sunnah ya Maghrib na Sunnah ya ´Ishaa alikuwa akiziacha safarini (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo muumini anatakiwa kufanya yale aliyokuwa akiyafanya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) safarini.

Inayozingatiwa safari kwa mujibu wa wanazuoni ni ile inayofikia katika umbali wake mchana na usiku. Hivi ndivo wanavoona jopo la wanazuoni wengi. Umbali huo unakisiwa kwa takriban 80 km kwa ambaye anasafiri kwa gari. Hali kadhalika kwa ndege, mtumbu na meli. Umbali huu na ule unaokaribiana nao ndio inaitwa ´safari` na ndio kwa mujibu wa desturi za watu wanazingatiwa kuwa ni safari. Ni jambo linalotambulika kati ya waislamu. Mtu akisafiri kwa ngamia, kwa miguu yake, kwa gari, kwa ndege au marikebu ya baharini, basi umbali huo au zaidi yake ni msafiri.

Wanazuoni wengine wakasema kikomo kinachozingatiwa ni desturi za watu na kigezo sio ule umbali unaopimwa kwa kilomita. Ile safari inayozingatiwa kuwa ni safiri kwa mujibu wa desturi za watu basi itaitwa safari na itafaa kufupisha na vinginevyo haitofaa.

Maoni ya sawa ni yale yaliyothibitishwa na kikosi kikubwa cha wanazuoni ambapo ni kuwekea kikomo cha umbali niliotaja. Hivi ndivo wanavoonelea wanazuoni wengi. Kwa hiyo inatakiwa kulazimiana na hilo. Jengine ni kwamba ndio jambo lililopokelewa kutoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ambao ndio watu wajuzi zaidi juu ya dini ya Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/266-267).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 32-34
  • Imechapishwa: 03/03/2022