95- Hakuna ubaya kuwazika ndani yake watu wawili au zaidi wakati wa dharurah. Atatangulizwa mbele yule mbora wao. Kumepokelewa Hadiyth kadhaa juu ya hilo:

Ya kwanza: Jaabir bin ´Abdillaah ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikusanya kati ya watu wawili [na watatu] katika wauliwa wa Uhud kwenye nguo moja kisha akiuliza: “Ni nani katika yao amechukua sehemu kubwa zaidi ya Qur-aan?” Akiashiriwa mmoja wao basi anamtanguliza ndani ya Lahd[1] [kabla ya mwenzake na anasema: “Mimi ni shahidi juu ya watu hawa siku ya Qiyaamah. Akaamrisha wazikwe ndani ya damu zao. Hakuwaosha na wala hakuwaswalia. [Siku hiyo akazikwa baba na ami yangu[2] ndani ya kaburi moja].”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/163-169, 07/300), an-Nasaa´iy (01/277) na at-Tirmidhiy (02/147). Ibn Maajah ameisahihisha (01/461), Ibn-ul-Jaaruud (270), al-Bayahqiy (04/14), Ahmad (05/431), ziada ya tatu ni yake na kwa al-Bukhaariy ambayo amepokea maana yake. Yeye al-Bukhaariy na al-Bayhaqiy wanayo ziada ya pili na Ibn Maajah anayo ya tatu. ash-Shawkaaniy (04/25) ameiegemeza kwa at-Tirmidhiy, jambo ambalo ni kosa.

Nusu ya pili ya Hadiyth kuna ziada ambayo imekwishatangulia katika masuala ya 32, uk. 54.

Ya pili: Abu Qataadah, ambaye amehudhuria hayo, amesimulia:

“´Amr bin al-Jamuuh alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unasemaje nikipambana katika njia ya Allaah mpaka nikauliwa – nitakuwa ni mwenye kutembea kwa mguu wangu mzima ndani ya Pepo?” Akuwa ni mlemavu wa miguu. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndio.” Akauliwa siku ya Uhud: yeye, mtoto wa kaka yake na mtumwa aliyeachwa huru. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapita karibu naye ambapo akasema: “Kama kwamba nakuangalia ukitembea kwa mguu wako huu ukiwa mzima Peponi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha wawili hao na yule mtumwa wao aliyeachwa huru kuwekwa ndani ya kaburi moja.”

Ameipokea Ahmad (05/299) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Hayo yamesemwa na al-Haafidhw (03/168).

Ya tatu: Jaabir amesimulia katika kisa ambacho baba yake alikufa shahidi kilichokwishatangulia, uk. 05, na mwishoni wame imekuja:

“… akawa ndiye muuliwa wa kwanza na akazikwa pamoja naye mwengine ndani ya kaburi moja… “

Kumepokelewa Hadiyth kutoka kwa Hishaam bin ´Aamir kuhusiana na maudhui haya. Hadiyth yake imekwishatangulia katika masuala ya 93, Hadiyth ya kwanza, uk. 141, kutoka kwa Anas bin Maalik. Imekwishatangulia katika masuala ya 37, uk. 59-60.

Katika Hadiyth kuna fadhilah za wazi juu ya msomaji wa Qur-aan:

al-Haafidhw amesema katika “al-Fath” (03/166):

“Wanaingia ndani yake wanachuoni, wenye kuipa nyongo dunia na njia zengine za fadhilah.”

ash-Shaafi´iy amesema katika “al-Umm” (01/245):

“Kutokana na ile dharurah, dhiki na haraka watazikwa ndani ya kaburi moja maiti wawili na watatu. Ambaye atakuwa upande wa Qiblah miongoni mwao ni yule mbora wao na mwenye umri mkubwa. Sipendi kwa hali yoyote azikwe mwanamke pamoja na mwanamme. Kama kumetokea dharurah na hakuna njia nyingine basi mwanamme atakuwa mbele ya mwanamke na mwanamke nyuma ya mwanamme. Baina ya mwanamme na mwanamke kutawekwa kizuizi cha udongo.”

[1] Bi maana katika kipande chake ijapo hakitofunika mwili mzima. Tazama taaliki 02, uk. 60.

[2] Dhahiri ni kwamba anakusudia ndugu yake baba yake, lakini mambo sivyo hivyo. Mkusudiwa ni ´Amr bin al-Jamuuh aliyetajwa katika Hadiyth baada yake. Alikuwa ni rafiki wa baba yake na Jaabir ambaye alikuwa mume wa dada yake Hind bint ´Amr. Ni kama kwamba Jaabir amemwita ami yake kwa sababu ya heshima, kama alivosema al-Haafidhw katika ”al-Fath” na akataja Aathaar inayotilia nguvu jambo hilo. Rejea (03/168).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 184-186
  • Imechapishwa: 03/03/2022