Kuhusu wakati ambao inatolewa Zakaat-ul-Fitwr ni kuanzia kuzama kwa jua usiku wa kuamkia siku ya ´iyd. Yule ambaye anawajibika kutoa anaweza kutoa kuanzia hapo, vinginevyo hapana. Kutokana na haya akifa kabla ya kuzama kwa jua, ijapo ni kabla ya dakika kadhaa, hatolazimika kutoa chakula. Akifa baada yake, ijapo ni dakika kadhaa baada yake, atawajibika kutolewa chakula. Mtoto mchanga akizaliwa baada ya kuzama kwake, ijapo ni kwa dakika kadhaa, haitolazimika kumtolea chakula, ingawa inapendeza kumtolea kama tulivyotangulia kusema. Akizaliwa kabla ya kuzama kwa jua, ijapo ni kwa dakika kadhaa, basi italazimika kumtolea chakula.

Hakika mambo yalivyo ni kwamba wakati wa kuwajibika kwake ni kuanzia kuzama kwa jua usiku wa kuamkia ´iyd kwa sababu ndio wakati ambao watu hufungua kutoka katika Ramadhaan. Kuongezea juu ya hayo kunasemwa yafuatayo: Msingi wa hukumu ya Zakaat-ul-Fitwr inatolewa kipindi hicho. Kuhusu wakati wa kutolewa kwake kuna nyakati mbili:

1 – Wakati ambao ni bora kuitoa.

2 – Wakati ambao inafaa kuitoa.

Kuhusu wakati ambao ni bora kuitoa ni asubuhi ya siku ya ´iyd kabla ya kuswaliwa. al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Tulikuwa tunaitoa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya kulisha [´Iyd] al-Fitwr pishi ya chakula.”

Imekuja katika Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha Zakaat-ul-Fitwr itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali.”

Ameipokea Muslim na wengineo.

Kwa ajili hiyo inapendeza watu kuchelewesha kuswali swalah ya ´Iyd-ul-Fitwr ili watu wapate muda wa kutosha wa kutoa chakula.

Kuhusu wakati ambao inafaa kuitoa ni siku moja au mbili kabla ya siku ya ´iyd.

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Naafiy´ aliyesema:

“Ibn ´Umar alikuwa akitoa kumpa mdogo na mkubwa mpaka alikuwa akitoa kwa niaba ya watoto wake. Alikuwa akiwapa wale wanaomjilia. Walikuwa wakipewa siku moja au mbili kabla ya [´Iyd] al-Fitwr.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 211-212
  • Imechapishwa: 23/03/2024