97. Imani kwa mtazamo wa Murji-ah na Radd juu yao

Kuhusu Murji-ah wanasema kwamba imani ni kule kusadikisha kwa moyo na kwamba matendo hayaingii ndani yake. Baadhi yao wanasema kuwa ni sharti ya ukamilifu. Baadhi yao wanasema ni sharti ya ulazima lakini haingii katika uhakika wa imani. Akiwa ni mwenye kusadikisha kwa moyo wake ni muumini hata kama hakufanya matendo. Haya ni madhehebu batili. Kwa sababu washirikina walikuwa wakitambua usahihi wa yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini pamoja na hivo walikataa kutamka shahaadah, wakakataa kuswali, kufunga, kutoa zakaah na kuhiji. Allaah (Ta´ala) amesema:

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”

Maneno Yake:

فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”[1]

Maana ya maneno haya ni kwamba wanamsadikisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini kilichowazuia ni kiburi, hasadi au kasumba kwa ajili ya dunia yao kutotamka shahaadah, kuswali, kufunga na kutoa zakaah. Lakini walikuwa wakifanya Hajj na wakifanya ´Umrah. Ni miongon mwa vile vitu vilivyobaki katika dini ya Ibraahiym. Lakini hawakuwa na zaidi ya hayo. Hajj yenyewe ilikuwa imeambatana na shirki. Walikuwa wakisema:

لبيك لا شريك لك إلا شريكا هو لك تملكه وما ملك

“Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia, huna mshirika Wewe, isipokuwa mshirika Wako ambaye unammiliki na anavyomiliki.”

Wakileta Talbiyah ya shirki. Kwa ajili hii ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alileta Talbiyah ya Tawhiyd kwa kusema:

لبيك لا شريك لك، إن الحمد والنعمة لك والملك لا شريك لك

”Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia, huna mshirika Wewe, nimekuitikia. Hakika himdi zote, neema na ufalme vyote ni Vyako. Hakika huna mshirika Wewe.”[2]

Amekanusha shirki ilihali wao walikuwa wakisema kuwa Allaah ana mshirika na wakiwaabudu badala ya Allaah na wakisema kwamba wao ndio waombezi wao mbele ya Allaah na wakatikati yao baina yao na mbele ya Allaah. Hali hii ni katika hajj.

Kuhusu swalah zao hawakuwa wakiswali, hawakuwa wakitoa zakaah, hawakuwa wakifunga na wala hawakuwa wakitamka shahaadah, lakini ndani ya mioyo yao walikuwa wakiamini kuwa ni Mtume wa Allaah. Walikuwa wakimsadikisha:

فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ

“Hakika wao hawakukadhibishi wewe.”[3]

Mayahudi na manaswara pia walikuwa wakisadikisha kuwa ni Mtume wa Allaah:

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ

“Wale Tuliowapa Kitabu wanamjua kama wanavyowajua watoto wao.”[4]

وَكَانُوا مِن قَبْلُ يَسْتَفْتِحُونَ عَلَى الَّذِينَ كَفَرُوا فَلَمَّا جَاءَهُم مَّا عَرَفُوا كَفَرُوا بِهِ ۚ فَلَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الْكَافِرِينَ

“… na japokuwa kabla ya hapo walikuwa wakiomba ushindi dhidi ya wale waliokufuru; basi yalipowajia yale waliyokuwa wakiyatambua waliyakanusha, basi laana ya Allaah iwe juu ya makafiri.[5]

Ndani ya mioyo yao walikuwa wakitambua kuwa ni Mtume wa Allaah. Lakini walikataa kutamka kwa ndimi zao na wakakataa vilevile kumfuata. Kusadikisha kwa mioyo hakukuwa kunatosha, kama wanavosema Murji-ah.

[1] 06:33

[2] al-Bukhaariy (1549) na Muslim (1184) kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[3] 06:33

[4] 02:146

[5] 02:89

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 135-136
  • Imechapishwa: 01/06/2021