96. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya imani

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naamini kwamba imani ni kutamka kwa ulimi, matendo ya viungo na kuamini ndani ya moyo. Inazidi kwa matendo mema na inapungua kwa maasi. Imani ni sabini na kitu. Ya juu yake kabisa ni “Laa ilaaha illa Allaah” na ya chini yake kabisa ni “kuondosha chenye kuudhi kutoka njiani.”

MAELEZO

Huu ni utangulizi wa utafiti wa imani. Ni jambo limekariri ndani ya Qur-aan sehemu nyingi na Allaah akawasifu watu wake na akawaahidi Pepo na thawabu tukufu.

Imani ni ngazi miongoni mwa ngazi za dini. Kwa sababu dini ni ngazi tatu, kama ilivyo katika Hadiyth ya Jibriyl: Uislamu, imani na Ihsaan.

Uislamu umejengeka katika zile nguzo tano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba ya Allaah tukufu. Haya ni matendo yenye kuonekana.

Imani imejengeka katika nguzo sita ambazo amezibainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, kufufuliwa baada ya kufa na kuamini Qadar kheri na shari yake.”

Ni lazima mambo haya yakusanyike kwa mja. Kwa msemo mwingine ni kwamba ni lazima Uislamu na imani vikusanyike kwa mja ambapo awe muislamu na muumini. Bi maana awe muislamu kwa uinje wake ambapo anatekeleza nguzo za Uislamu. Vilevile awe muumini kwa undani wake ambapo anaamini nguzo hizi sita. Asiwe ni muislamu peke yake pasi na imani. Hii ndio hali ya wanafiki ambao wanadhihirisha Uislamu kwa uinje wao ambapo wanaswali, wanafunga, wanatamka shahaadah na wanahiji. Lakini hawana imani ndani ya moyo:

يَقُولُونَ بِأَفْوَاهِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ

”Wanasema kwa midomo yao yale yasiyokuwemo katika nyoyo zao.”[1]

Hawa wako katika tabaka la chini kabisa Motoni. Vivyo hivyo kinyume chake. Mtu asiwe ni muumini bila ya Uislamu kwa njia ya kwamba akawa ni mwenye kusadikisha na ni mwenye kuamini nguzo hizi kwa moyo wake. Lakini hata hivyo hana Uislamu; haswali, hatoi zakaah, hafungi wala hahiji. Huyu sio muumini mpaka awe muislamu mwenye kutekeleza nguzo za uinje na za undani. Ni lazima jambo hilo. Imani ni mkusanyiko wa imani za moyo, matendo ya viungo na kutamka kwa ulimi. Kwa ajili hiyo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, kama alivotaja Shaykh, wanasema:

“Imani ni kutamka kwa ulimi, kuamini ndani ya moyo ma matendo ya viungo.”

Ni lazima yapatikane mambo haya matatu:

1- Kutamka kwa ulimi.

2- Kuamini ndani ya moyo.

3- Matendo ya viungo.

Inazidi kwa matendo mema na inapungua kwa maasi. Hii ndio maana ya imani kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambao ndio wenye kufuata Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ambao ndio kundi lililookoka kati ya mapote potofu ambayo Allaah ameyatishia kuingia Motoni. Hii ndio imani kwa mujibu wao na imejengeka katika vitu hivi vitatu.

[1] 03:167

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 134-135
  • Imechapishwa: 01/06/2021