Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

76 – Matendo huzingatiwa ule mwisho wake.

MAELEZO

Mtu kamwe asighurike kwa matendo yake pasi na kujali ni mwema kiasi gani. Bali anatakiwa kuogopa mwisho mbaya. Hatakiwi kumuhukumu yeyote kuwa ni mtu wa Motoni kutokana na matendo yake, kwa sababu hajui mwisho wake atamalizia vipi. ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arobaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu. Kisha huwa donge la damu kwa muda kama huo. Kisha huwa pande la nyama kwa muda kama huo. Kisha Allaah humtumia Malaika na akampulizia roho na akaamrishwa aandike maneno manne; riziki yake, muda wake wa kuishi, matendo yake na kama atakuwa mtu muovu au mwema. Naapa ambaye hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye! Hakika mmoja wenu atafanya matendo ya watu wa Peponi mpaka kusiwe kati yake yeye na hiyo isipokuwa dhiraa akatanguliwa na kitabu ambapo akafanya matendo ya watu wa Motoni na akaingia ndani yake. Na hakika mmoja wenu atafanya matendo ya watu wa Motoni mpaka kusiwe kati yake yeye na hiyo isipokuwa dhiraa akatanguliwa na kitabu ambapo akafanya matendo ya watu wa Peponi na akaingia ndani yake.”[1]

Mtu anatakiwa kuogopa mwisho mbaya na wala asimuhukumu yeyote kwamba atapata mwisho mbaya kwa sababu hajui ni vipi atayamaliza maisha. Tawbah inafuta madhambi yaliyotangulia:

قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ

“Waambie wale waliokufuru kwamba wakikoma watasamehewa yaliyotangulia.”[2]

Matendo yanazingatiwa ule mwisho wake. Lakini miongoni mwa upole wa Allaah (´Azza wa Jall) kwa waja Wake ni kwamba yule ambaye aliishi akiwa mwema basi humaliza maisha yake akiwa mwema, na yule ambaye aliishi akiwa muovu basi humaliza maisha yake akiwa muovu. Kwa hivyo mtu anatakiwa kufanya sababu na amjengee dhana nzuri Allaah (´Azza wa Jall). Baadhi ya watu wanafikiri kuwa watatubu kabla ya wao kufa. Hivi unajua ni lini utakufa? Pengine ukafa katika wakati ambapo hutowahi kutubia. Jengine ni kwamba hawajui kama tawbah zao zimekubaliwa au hazikukubaliwa, kwa sababu tawbah ina sharti zake.

[1] al-Bukhaariy (6549) na Muslim (2643).

[2] 8:38

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 110-111
  • Imechapishwa: 30/10/2024