93. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu Bid´ah na Ahl-ul-Bid´ah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naona kuwahama na kuwatenga Ahl-ul-Bid´ah mpaka watubie. Nawahukumu kwa uinje na nazitegemeza siri zao kwa Allaah. Naamini kwamba kila kilichozuliwa katika dini ni Bid´ah.

MAELEZO

Bid´ah ni yale yaliyozuliwa ndani ya dini katika ´ibaadah ambazo hazina dalili kutoka katika Qur-aan wala Sunnah. Kwa sababu ´ibaadah ni Tawqiyfiyyah. Hiyo ina maana kwamba hatufanyi kitu katika hayo isipokuwa kwa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Mwenye kuja na akazua jambo ambalo anajikurubisha kwalo mbele ya Allaah katika kumtaja Allaah, kuswali au ´ibaadah na akasema kuwa ni nyongeza na kwamba haina ubaya wowote, tunampinga na kumwambia kwamba nyongeza hii ni shari na haina kheri yoyote. Kwa sababu dini imekamilika na haikubali nyongeza na mambo ya ziada. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekufa baada ya kuwa dini imekwishakamilika. Amesema (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

“Leo nimekukamilishieni dini yenu.”[1]

Allaah ameshuhudia kwamba dini hii imekamilika. Kwa hiyo haikubali ziada na mambo ya nyongeza. Inatutosha kutendea kazi zile ´ibaadah zilizomo katika dini hii. Ama kuzidisha na kusema kuwa ziada hii ni ya kheri ni jambo la Bid´ah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika yule miongoni mwenu atakayeishi kipindi kirefu basi ataona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo yaliyozuliwa. Kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

Katika Khutbah zake alikuwa akisema:

“Amma ba´d: Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kila Bid´ah ni upotevu.”[2]

Hapa kuna Radd juu ya wale wanaogawanya kati ya Bid´ah nzuri na Bid´ah mbaya. Hakuna kitu kizuri juu ya Bid´ah katika dini. Bali zote ni mbaya. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila Bid´ah ni upotevu.”

Mzushi huyu anasema:

“Sio kila Bid´ah ni upotevu. Bali zipo Bid´ah nzuri.”

Huyu anamjibu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mshairi amesema:

“Ubora wa mambo ni yale yaliyopita juu ya uongofu. Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kuanzishwa.”

Wale wanaosema kuwa kuna Bid´ah nzuri wanatakiwa kuambiwa kwamba Bid´ah hizo ni ovu na mbaya na sio nzuri. Ndani ya dini hakuna Bid´ah nzuri kabisa. Kwa hivyo tunapaswa kujiepusha na Bid´ah na kukomeka na Sunnah. Ndani yake kuna kheri na ukamilifu.

[1] 05:03

[2] Muslim (867) kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiy Allaahu ´anhumaa).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 131-132
  • Imechapishwa: 31/05/2021