92. Njia tatu za Kishari´ah za mtu kuwa kiongozi katika Uislamu

Maneno yake:

“Yule ambaye atatawala na watu wakakusanyika juu yake, wakamridhia na akawashinda kwa upanga wake mpaka yeye akawa ndiye khaliyfah, basi ni lazima kumtii.”

Hili ni moja ya mambo ambayo yanafungika uongozi.

Wanachuoni wamesema kuwa uongozi unasimama kwa moja ya mambo matatu:

1- Ahl-ul-Hall wal-´Aqd kumchagua. Ahl-ul-Hall wal-´Aqd wakimchagua na wakampa bay´ah basi ni lazima kumtii. Ni kama mfano wa ukhaliyfah wa Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) ulithibiti kwa kuchaguliwa na Ahl-ul-Hall wal-´Aqd. Si lazima waislamu wote wamchague kama inavyofanywa katika upigaji kura. Hii sio nidhamu ya Kiislamu. Bali inatosha kwa Ahl-ul-Hall wal-´Aqd katika wanachuoni, viongozi, watu wa mitazamo na mashauriano. Wakichagua mtawala wa waislamu basi ni lazima kwa waislamu wote kumtii. Haifai kwa yeyote kusema kuwa yeye hakuchagua na kwamba hakula kiapo cha usikivu, kama wanavosema baadhi ya wajinga hii leo. Wewe ni mmoja katika waislamu na waislamu wamemchagua mtu huyu kuwa ni mtawala wao. Kwa hiyo haijuzu kwako kwenda kinyume na kutoka nje yao. Bali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Waislamu ni mkono juu ya wengine. Dhimma ya wa chini yao inawaenea wengine.”[1]

Ikiwa dhimma ya wa chini wao inawaenea wengine, vipi tusemeje juu ya Ahl-ul-Hall wal-´Aqd, watu wa mashauri na wa mitazamo? Maswahabah walimtii Abu Bakr pamoja na kwamba waliompa kiapo cha usikivu ni wale viongozi wa Muhaajiruun na Answaar katika ukumbi wa Banuu Saa´idah. Vivyo hivyo ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) alichaguliwa na watu wa mashauri sita ambao waliteuliwa na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh). Aliwateua wale kumi waliobaki ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikufa na yeye yuko radhi nao. Watu sita maoni yako yaliyomchagua ´Uthmaan ambapo wakampa kiapo cha usikivu. Hivyo waislamu wote wakalazimika kumtii.

2- Uteuliwaji wa anayekuja baadaye. Mtawala akimteua mwengine baada yake ni lazima kumtii na uongozi wake unafungika. Ni kama ambavo Abu Bakr alimteua ´Umar ambapo wakamsikiliza na kumtii (Radhiya Allaahu ´anhum).

3- Watu wakiwa hawana kiongozi ambapo akasimama mtu ambaye ana ushujaa na nguvu na akawashinda watu kwa upanga wake mpaka wakanyenyekea kwake, huyu ni lazima kumtii. Wanapigia mfano wa hili kwa ´Abdul-Malik bin Marwaan. Watu katika wakati wake walikuwa hawana kiongozi wa nchi nzima. Bwana huyu akasimama kwa ujasiri, ukuu na nguvu ambapo akapambana na akashinda ambapo waislamu wakamtii. Akawa ni mtawala wao na uongozi wake ukasimama kwa jambo hilo.

Ama ambaye anakuja na waislamu tayari wameshakuwa na mtawala na kuvutana na mtawala na akataka kumg´oa mtawala huyo ili yeye ndiye ashike nafasi yake, huyu ni lazima kwa waislamu kumpiga vita. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayekujieni na jambo lenu ni moja juu ya mtu mmoja anataka kuvunja umoja au kufarikisha mkusanyiko wenu, mpigeni vita – vovyote awavyo.”[2]

Sisi tuko upande wa mtawala. Ataposimama mmoja basi sisi tuko pamoja naye katika kumzuia Khaarijiy huyu dhidi ya umoja wa waislamu. Tunampiga vita na kutokomeza shari yake dhidi ya waislamu ili asivunje umoja na hayo ni kwa ajili ya manufaa ya jumla.

Hii ndio ´Aqiydah ya Shaykh kuhusu kuwasikiliza na kuwatii watawala wa waislamu. Hapa kuna Radd kwa wale wanaomsifu kufanya uasi dhidi ya watawala.

[1] Abu Daawuud (4530), an-Nasaa´iy (4734), Ahmad katika ”al-Musnad” (01/119 nambari. 959) kupitia kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

Msingi wake uko kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia Hadiyth ya ´Aliy kwa tamko lisemalo:

”Dhimma ya waislamu inamwenea mpaka yule wa chini.”

Ameipokea al-Bukhaariy (7300) na Muslim (1370).

[2] Muslim (1852).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 129-130
  • Imechapishwa: 31/05/2021