Lakini Jihaad ina sharti:

1 – Sharti ya kwanza: Waislamu wawe na nguvu ambazo wanaweza kupambana na makafiri. Kwa msemo mwingine wawe na matayarisho na maandalizi juu ya kupambana na makafiri. Wasipokuwa na maandalizi ya kutosha, kwa mfano wana unyonge fulani na makafiri wana nguvu zaidi kuliko wao, na endapo waislamu watawapiga vita makafiri basi litawasababishia madhara waislamu. Katika hali hii vita havitojuzu. Kwa sababu jambo hili litasababisha madhara makubwa kuliko manufaa. Nayo ni kwamba makafiri watawashambulia waislamu. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alibaki Makkah kwa miaka kumi na tatu akifupika na kulingania katika dini ya Allaah peke yake. Kipindi hicho waislamu walikuwa wakiudhiwa, wakinyongeshwa na hakuamrishwa Jihaad. Bali Allaah alimwamrisha kufanya subira, kujizuia mikono yake mpaka pale Allaah (Jalla wa ´Alaa) alipomuidhinisha Jihaad:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ قِيلَ لَهُمْ كُفُّوا أَيْدِيَكُمْ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ

“Je, huoni wale walioambiwa zuieni mikono yenu na simamisheni swalah na toeni zakaah.”[1]

Hapa ni Makkah. Waliamrishwa kuizuia mikono yao. Lakini pamoja na hivo walinganie katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipohajiri kwenda Madiynah na Uislamu ukaenea na waislamu wakawa na nguvu ndipo Allaah akamwamrisha Jihaad. Kwa sababu wakati huo walikuwa na nguvu na wako tayari kwa ajili ya Jihaad. Jambo hili halihusu ule wakati wa mwanzo peke yake. Hili ni jambo lenye kuenea kwa waislamu mpaka zama za mwisho. Wakiwa na nguvu na uwezo basi ni lazima kwao kulingania katika kufanya Jihaad. Wakiwa hawana nguvu basi watatakiwa kubaki wakilingania. Kuhusu Jihaad wataichelewesha mpaka katika wakati watapokuwa na uwezo wake. Kwa sababu wakipigana ilihali ni wadhaifu makafiri watawashambulia na kuwashinda.

2 – Sharti ya pili: Jihaad iwe chini ya uongozi unaoongozwa na mtawala wa waislamu. Si kila mmoja anapigana Jihaad na vita kivyake na kila mmoja anakuwa na kikundi chake. Hili ni jambo lisilojuzu katika Uislamu. Haya madhara yake yako kwa waislamu wenyewe kabla ya kuwadhuru makafiri. Kwa sababu waislamu wanachukiana kati yao. Kila mmoja anataka aonekane ndiye mwenye natija nzuri. Haya yamejaribiwa juu ya vikundi vilivyowapiga vita maadui. Wakati adui aliposhindwa wakaanza kupigana wao kwa wao; kila mmoja anataka yeye ndiye ashike uongozi. Hii ndio natija kwamba hawakupigana chini ya uongozi na mtawala mmoja. Wamefarikiana katika vikundi na vyama. Kitendo hichi hakijuzu ndani ya Uislamu. Ni lazima Jihaad iwe chini ya uongozi mmoja. Kwa ajili hii Shaykh amesema:

“Naona Jihaad ni yenye kuendelea pamoja na kila kiongozi.”

Bi maana mtawala wa waislamu ambaye anawaongoza, anawapangilia, anawasimamia na anawafanyia maandalizi ya kisilaha. Ni lazima Jihaad iwe chini ya uongozi mmoja na kwa amri yake ili Jihaad itoe natija nzuri. Ama ikiwa ni pasi na kiongozi na bila ya uongozi basi mwishowe inapelekea katika kushindwa. Maneno yake:

“… pamoja na kila kiongozi.”

ni dalili inayoonyesha kuwa kuwepo kwa kiongozi ambaye watu wanapambana chini ya uongozi wake ni sharti. Si sharti kiongozi huyo awe mwema mia kwa mia kama mfano wa Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy, ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz na Maswahabah wengine. Si sharti kiongozi awe msafi na asiwe na kasoro. Bali hata akiwa muovu na mtenda madhambi, ambayo hayajamfikisha katika kiwango cha ukafiri, midhali uongozi wake ni wenye kubaki bado anastahiki kuongoza Jihaad, anatiiwa katika Jihaad na watu wanaswali nyuma yake kwa sababu bado ni muislamu ijapokuwa ni muasi, mtenda madhambi, mkandamizi na mwenye kudhulumu. Kwa sababu manufaa katika kukuanyika ni yenye nguvu zaidi kuliko kufarakana na kutofautiana juu yake.

[1] 04:77

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 120-122
  • Imechapishwa: 25/05/2021