86. Wanaharakati na wenye hamasa hawastahamili haya kwa sababu ni wajinga

Masuala haya makubwa wanapumbaa kwayo watu wengi wenye hamasa ambao hawana uelewa wowote katika dini. Wanahoji ni vipi watamuasi ilihali ni mtenda madhambi na maasi? Tunamjibu kwa ajili ya manufaa kwa jumla. Kufanya dhara dogo kwa ajili ya kuepuka dhara kubwa ni jambo linalotakikana katika Uislamu. Kuyazuia madhara ni jambo linalotangulizwa mbele ya kuleta manufaa. Waislamu walipigana vita bega kwa bega pamoja na al-Hajjaaj na pamoja na Yaziyd bin Mu´aawiyah ilihali ni watenda madhambi. Yote hayo kwa ajili ya umoja. Bali katika uongozi wa Yaziyd bin Mu´aawiyah walikuweko Maswahabah katika vita vya Constantinople. Mmoja wapo ni Abu Ayyuub al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh). Kadhalika walipigana vita bega kwa bega pamoja na al-Hajjaaj naye alikuwa anatambulika kwa dhuluma. Alikuwa ni dhalimu, mwaga damu na mkandamizi. Lakini kwa ajili ya manufaa ya Uislamu na waislamu. Masuala madogo yanasamehewa pindi yanapokabiliana na manufaa yenye kuenea kwa watu wote. Hii ni kanuni ya Kiislamu.

Kwa hiyo si sharti kiongozi anayesimamia mambo ya waislamu na anawaongoza katika Jihaad awe mwema na mwenye kunyooka mia kwa mia. Bali hata kama atakuwa na kitu katika maasi na mambo yanayokwenda kinyume muda wa kuwa hajamfikisha katika kiwango cha kumkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Lakini wajinga wenye hamasa hawastahamili maneno haya. Kwa sababu ni wajinga. Maswahabah walistahamili na wakamtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hilo kwa sababu ya uelewa na imani yao. Ama wajinga na wenye hamasa hawawezi kuyatashamili haya. Wale wenye malengo yao pia hawastahamili haya. Ni watu ambao huenda si wajinga wanayajua haya. Lakini ni wenye malengo yao wanachotaka ni kuwafarikisha waislamu. Matokeo yake wanachochea dhidi ya watawala kwa sababu eti watawala wanafanya mambo ambayo ni ya makosa. Yote hayo kwa ajili ya kufarikisha umoja na kuwadhoofisha waislamu. Kwa hiyo ni lazima kuyaelewa mambo haya, kutahadhari nayo na kutoyakimbilia bila ya uelewa na elimu. Haya ni masuala makubwa ambayo hii leo watu wamekuwa na ufahamu wa kimakosa na kuwapotosha watu kwa sababu ima ya ujinga au matamanio.

Maneno yake:

“Mwema.”

ni yule mwema aliyenyooka.

Maneno yake:

“Muovu.”

Ni yule mtenda madhambi lakini hata hivyo hajafikia kiwango cha ukafiri. Kwa sababu manufaa katika kumtii na kupigana Jihaad bega kwa bega pamoja naye ni yenye nguvu zaidi kuliko madhara katika kufanya subira juu ya madhambi yake.

Maneno yake:

“Inafaa kuswali swalah ya mkusanyiko nyuma yao.”

Hapana shaka kwamba kuswali nyuma ya viongozi watenda madhambi ni jambo linalofaa na swalah ni sahihi. Midhali wanaswali basi wewe swali nyuma yao. Maswahabah waliswali nyuma ya al-Hajjaaj, wakaswali nyuma ya ´Abdullaah bin Ziyaad na wakaswali nyuma ya watawala watenda madhambi ambao wanakunywa pombe. Kadhalika wakaswali nyuma ya al-Waliyd bin ´Uqbah. Waliswali nyuma yao kwa ajili ya kuleta umoja. Isitoshe hawa ni waswali swalah zao zinasihi. Muda wa kuwa swalah zao zinasihi uimamu wao unasihi kwa ajili ya kuleta umoja.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 122-123
  • Imechapishwa: 25/05/2021