83. Ibn ´Abdil-Wahhaab ´Aqiydah yake hawakufurishi waislamu

Amesema (Rahimahu Allaah):

“Simkufurishi yeyote katika waislamu kwa dhambi na wala simtoi katika mduara ya Uislamu.”

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwamba hawakufurishi kwa madhambi makubwa yaliyo chini ya shirki. Kwa mfano wa uzinzi, kuiba, kunywa pombe na kula ribaa. Haya ni madhambi makubwa yanayoangamiza. Lakini hata hivo hawamhukumu mwenye nayo ukafiri. Bali wanamhukumu kuwa na imani pungufu. Ni madhambi makubwa yanayoipunguza imani. Mwenye nayo anahukumiwa kwamba yuko chini ya utashi wa Allaah; akitaka atamuadhibu na akitaka atamsamehe:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

 “Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Sisi hatumkufurishi isipokuwa aliyekufurishwa na Allaah na Mtume Wake kwa dalili kutoka kaitka Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya wanachuoni.

Ama kukufurisha kwa madhambi makubwa yaliyo chini ya shirki ni madhehebu ya Khawaarij na Mu´tazilah wapotevu ambao wanamhukumu mwenye kufanya dhambi kubwa ya kwamba ni kafiri na kwamba ni mwenye kudumishwa Motoni milele. Tunamuomba Allaah afya. Hii ni ´Aqiydah batili inayopingana na dalili.

Lakini ambaye atahalalisha jambo la haramu ambalo kuna maafikiano juu ya uharamu wake ni kafiri. Kama kwa mfano akahalalisha ribaa, pombe, uzinzi au akaharamisha kitu ambacho kuna maafikiano juu ya uhalali wake hapo mtu huyo atakuwa ni kafiri. Kwa sababu atakuwa ni mwenye kumkadhibisha Allaah, Mtume Wake na maafikiano ya waislamu. Masuala ya kukufurisha yana vidhibiti vyake kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ama kufanya dhambi kubwa iliyo chini ya shirki hapana shaka kwamba ni jambo la khatari. Mtu huyo amepewa matishio ya Moto na ghadhabu. Lakini hata hivyo hatumhukumu ukafiri. Bali tunasema kuwa ni muumini mwenye imani pungufu. Kuna khatari huko Aakhirah akaingia ndani ya matishio yaliyopokelewa. Allaah akitaka atamsaemehe na akitaka atamuadhibu. Lakini akimuadhibu hatodumishwa Motoni milele kama makafiri. Bali atatoka na kwenda Peponi. Hatoki katika mduara wa Uislamu. Bali anabaki ndani ya mduara wa Uislamu. Anakuwa pamoja naye na msingi wa Uislamu na imani. Lakini imani yake inakuwa dhaifu. Kwa sababu imani inaipunguza imani.

Tazama maneno ya imamu huyu ambaye wapinzani wake wamesema juu yake kwamba anawakufurisha waislamu. Yeye mwenyewe amejikanushia tuhumu hii batili na amebainisha yale anayoonelea.

[1] 04:116

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 116-117
  • Imechapishwa: 25/05/2021