82. Dalili ya nguzo ya kwanza ambayo ni shahaadah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya Shahaadah ni Kauli Yake (Ta´ala):

شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah ameshuhudia kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Malaika na wenye elimu [pia wameshuhudia], ni Mwenye kusimamisha kwa uadilifu. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mwenye hekima.”[1]

MAELEZO

Kushuhudia… – Maana yake ni kwamba amehukumu, ameamua, kutangaza, amebainisha na kulazimisha. Shahaadah kutoka kwa Allaah kunazunguka juu ya maana hizi tano: hukumu, kuamua, kutangaza, kubainisha na kulazimisha. Maana ya kushuhudia ni kwamba Yeye (Subhaanah) ametangaza, akakhabarisha na akawalazimisha waja Wake jambo hilo kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Yeye.

Hapana mungu wa haki – Ukanushaji hapa ni wenye kukanusha yale yote yenye kuabudiwa badala ya Allaah.

Isipokuwa Yeye – Ni yenye kuthibitisha ´ibaadah kwa Allaah pekee. Maana ya kwamba hapana mungu isipokuwa Yeye ni kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kuhusu ambaye anamwabudu mwengine asiyekuwa Allaah basi ´ibaadah yake ni batili kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Mkubwa.”[2]

Ameshuhudia juu ya nafsi Yake (Subnaahahu wa Ta´ala) upwekekaji – Naye ndiye mkweli mno wa wazungumzaji. Ushuhuda Wake ndio ushuhuda wenye ukweli zaidi. Kwa sababu ni ushuhuda wenye kutoka kwa Mwingi wa hekima, Mwenye khabari zote na mjuzi wa yote. Anakijua kila kitu. Kwa hiyo ni ushuhuda wenye ukweli kabisa.

Na Malaika –  Wameshuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah. Hawa ni walimwengu walioumbwa na Allaah kwa ajili ya kumwabudu. Malaika ni waja watukufu walioumbwa na Allaah ili wamwabudu Yeye. Wanamtukuza usiku na mchana hawachoki. Vilevile Allaah amewaumba ili watekeleze maamrisho Yake juu ya ulimwengu. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) amewapa kazi ya kutekeleza yale anayowaamrisha katika mambo ya ulimwenguni. Kila Malaika amepewa kazi yake. Ushuhuda wao ni wa kweli. Kwani wao ni wakweli, viumbe wenye ´ibaadah  na wenye kumtambua Allaah (´Azza wa Jall). Wao ndio viumbe bora pamoja na tofauti ilioko kama watu wema ndio bora kuliko Malaika au Malaika ndio bora kuliko watu wema? Wanachuoni wametofautiana juu ya hili.

Wenye elimu – Wamegawanyika aina mbili:

Ya kwanza: Malaika.

Ya pili: Watu.

Wenye elimu hawatoi ushuhuda isipokuwa kwa ambayo ni ya haki. Hayo ni tofauti na watu ambao ushuhuda wao hauzingatiwi. Kila mwenye elimu aliyeumbwa na Allaah anamshuhudilia Allaah juu ya umoja na kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Yeye. Hapa kuna utukufu kwa wanachuoni kwa sababu Allaah ameambatanisha ushuhuda wao pamoja na usuhuda Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) na ushuhuda wa Malaika Wake. Amezingatia ushuhuda wa wenye elimu katika watu. Hiyo imefahamisha juu ya ubora wao, utukufu wao na nafasi yao juu ya kitu kitukufu zaidi ambacho ni Tawhiyd.

[1] 03:18

[2] 22:62

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 163-165
  • Imechapishwa: 06/01/2021