83. Makusudio ya neno ´wasomi` waliokusudiwa katika Qur-aan na Sunnah

Makusudio ya “wenye elimu” ni wale wenye elimu ya Shari´ah. Mambo si kama wanavosema baadhi ya watu kwamba makusudio ya wale wenye elimu ni wale wavumbuzi na wakulima. Hawa hawaitwi kuwa ni wasomi kwa njia ya kuachia. Kwa sababu elimu yao ni yenye mpaka na imefungamanishwa. Bali husemwa ´huyu ni msomi wa hesabu, msomi wa uhandisi, msomi wa udaktari`. Hawaitwi kuwa ni wasomi kwa njia ya kuachia. Wenye kuitwa hivo ni wale wanachuoni wa dini.

Isitoshe wengi miongoni mwa hawa watu ni wale waliosoma elimu ya kidunia na ndani yake wamo wakanamungu ambao mara nyingi elimu yao inawazidishia kumjahili Allaah (´Azza wa Jall) na ukafiri. Hayo mnayashuhudia wenyewe hii leo katika jamii za kikafiri. Wameendelea katika mambo ya viwanda na kilimo lakini hata hivyo ni makafiri. Ni vipi basi mtu anaweza kusema kuwa wao ndio wasomi ambao wametajwa na Allaah pale aliposema:

 وَأُولُو الْعِلْمِ

“.. na wenye elimu [pia wameshuhudia]… “

Hili ni jambo lisiloingia akilini kabisa. Vivyo hivyo pale aliposema:

Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ

“Hakika si vyenginevyo wanaomkhofu Allaah miongoni mwa waja Wake ni wanazuoni.”[1]

Makusudio ni wanachuoni wa dini ambao wanamtambua Allaah ipasavyo, wanamwabudu na kumcha Allaah ipasavyo. Ama watu wa upande wa pili wengi wao hawamchi Allaah (´Azza wa Jall). Bali wanamkufuru na kumkanusha Allaah na wanadai kuwa ulimwengu hauna mola. Wanaona kuwa mazingira ndio yaliyowaumba na ndio yanayoendesha ulimwengu. Hivo ndivo hali ilivyo kwa wakomunisti. Wanampinga Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) pamoja na kwamba wana elimu ya kidunia. Ni vipi tutasema kuwa hawa ni wanachuoni na wasomi? Hili ni kosa. Neno ‘elimu` halitumiwi isipokuwa kwa wenye kulistahiki. Ni neno ambalo ni tukufu. Halitumiwi kwa wakanamungu na makafiri na mtu akadai kuwa wao ndio wanachuoni.

Malaika na wanachuoni wamemshuhudilia Allaah juu ya umoja. Kwa hivyo hayazingatiwi maneno ya wengine katika wakanamungu, washirikina na makafiri wengine ambao wanamkufuru Allaah hayazingatiwi. Watu aina hii wanapuuzwa na maneno yao pia yanapuuzwa. Kwa sababu ni wenye kupingana na ushuhuda wa Allaah, ushuhuda wa Malaika na ushuhuda wa wanachuoni katika viumbe Wake.

Uadilifu ni kinyume cha jeuri. Yeye (Subhaanah) ni mwenye kuhukumu kwa uadilifu. Hakuna kinachotoka Kwake isipokuwa uadilifu mtupu katika kila kitu.

Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye – Ni kutilia nguvu sentesi ya kwanza.

Mwenye nguvu kabisa asiyeshindikana, Mwenye hekima – Ni majina mawili ya Allaah (´Azza wa Jall). Ndani yake mna sifa mbili miongoni mwa sifa Zake ambazo ni nguvu zisizoshindika, hekima.

Mwenye kusimamisha – Bi maana hali ya kuwa ni mwenye kusimamisha.

Uadilifu – Bi maana Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni mwenye kusimamisha uadilifu katika kila kitu.

[1] 35:28

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 165-166
  • Imechapishwa: 06/01/2021