Isti´aanah: Ni kule kutaka msaada kutokana na jambo.

Istighaathah: Ni kule kuomba uokozi na kuondosha matatizo.

Kuna aina mbili za kuwataka msaada na uokozi viumbe:

Ya kwanza: Kuwaomba msaada na uokozi viumbe katika mambo wanayoyaweza. Kitendo hichi kinafaa. Amesema (Ta´ala):

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ

“Saidianeni katika wema na kumcha Allaah.”[1]

Amesema (Ta´ala) katika kisa cha Muusa (´alayhis-Salaam):

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ

“Akamsaidia yule ambaye ni katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake.”[2]

Vilevile kama ambavo mtu anamtaka msaada mwenzake vitani na kwenginepo katika mambo ambayo viumbe wanayaweza.

Ya pili: Kuwaomba msaada na uokozi viumbe katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah pekee. Kama mfano wa kuwaomba msaada na uokozi wafu. Vilevile kuwaomba msaada na uokozi viumbe waliohai katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah kama vile kuwaponya wagonjwa, kuwaondoshea matatizo na kuwazuilia madhara. Aina hii haijuzu. Ni shirki kubwa.

Katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwepo mnafiki anayewaudhi waumini. Baadhi yao wakasema: “Hebu twende tumtake uokozi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokamana na mnafiki huyu.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Uokozi hauombwi kutoka kwangu. Uokozi unaombwa kutoka kwa Allaah.”[3]

Kuchukia kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutumia tamko hili juu yake – ijapokuwa ni katika mambo anayoyaweza katika uhai wake – ni kwa sababu ya kuilinda Tawhiyd na kufunga njia inayopelekea katika shirki, kuonyesha adabu na kunyenyekea mbele ya Mola Wake na kuutahadharisha Ummah wake kutokamana na njia za shirki katika maneno na vitendo. Ikiwa hali ndio hii katika jambo analoliweza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maisha yake, vipi atakwe uokozi baada ya kufa kwake na aombwe mambo asiyoyaweza yeyote isipokuwa Allaah pekee[4]? Ikiwa jambo hili halijuzu juu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi kwa mwengine kutakuwa kuna haki zaidi ya kutokufaa.

[1] 05:02

[2] 28:15

[3] Ahmad (22758). al-Haythamiy ameinasibisha kwa at-Twabaraaniy na akasema katika “Majma´-uz-Zawaaid” (11/26):

”Wanaume wake ni wanaume Swahiyh isipokuwa tu Ibn Lahiy´ah. Ni Hadiyth nzuri.”

[4] Fath-ul-Majiyd, uk. 196-197.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 146-147
  • Imechapishwa: 11/06/2020