2- Tawassul isiyokubali Kishari´ah. Tawassul aina hii ni kufanya Tawassul mbali na zile zilizotajwa katika aina ya kwanza katika Tawassul inayokubalika Kishari´ah. Kama mfano wa kufanya Tawassul kwa kuwaomba wafu du´aa na uombezi, kufanya Tawassul kwa jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kufanya Tawassul kwa dhati za viumbe na haki zao. Upambanuzi wa hayo ni kama ifuatavyo:

a) Kuomba du´aa kutoka kwa wafu haijuzu. Kwa sababu maiti hawezi kuomba du´aa kama alivyokuwa anaweza wakati alipokuwa hai. Vilevile haijuzu kuwaomba uombezi wafu. Kwa sababu ´Umar bin al-Khattwaab, Mu´aawiyah bin Abiy Sufyaan (Radhiya Allaahu ´anhumaa) na Maswahabah wengine waliokuwa wakati wao na wale waliowafuata kwa wema waliposhikwa na ukame wakaenda kuomba du´aa ya kuteremshiwa mvua kutoka kwa wale waliokuwa hai, kama mfano wa ´Abbaas na Yaziyd bin al-Aswadiy, hawakufanya Tawassul, hawakuomba uombezi wala kuomba kuteremshiwa mvua kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); si kwenye kaburi lake wala kaburi la mwengine. Bali walimwendea mtu mwengine badala yake, kama al-´Abbaas na al-Yaziyd. ´Umar alisema:

“Ee Allaah! Hakika sisi tulikuwa tukifanya Tawassul Kwako kupitia Mtume wetu ukituteremshia mvua na hivi sasa tunafanya Tawassul kwa ami yake Mtume wetu, hivyo tuteremshie mvua.”

Akafanya haya badala ya yale baada ya kushindwa kufanya Tawassul kwa njia inayokubalika katika Shari´ah ambayo hapo kabla walikuwa wakiifanya. Kulikuwa kuna uwezekano kwake kuliendea kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakafanya Tawassul kupitia kwake[1]. Namaanisha endapo ingelikuwa inafaa. Lakini kuacha kwao kufanya hivo ni dalili inayoonyesha kutofaa kufanya Tawassul kupitia wafu kwa kuwaomba du´aa na uombezi kutoka kwao. Lau kitendo cha kuomba du´aa na uombezi kutoka kwake akiwa hai na maiti ingelikuwa ni sawasawa basi asingemwacha na kumwendea mwengine ambaye yuko chini yake.

b) Kufanya Tawassul kwa jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au jaha ya mtu mwengine haijuzu. Hadiyth inayosema:

‏إذا سألتم الله فاسألوه بجاهي، فإن جاهي عند الله عظيم

“Mnapomuomba Allaah basi muombeni kwa jaha yangu. Kwani hakika jaha yangu mbele ya Allaah ni kubwa.”

ni Hadiyth iiliyozuliwa. Ndani yake hakuna kitu katika vitabu vya waislamu vinavyotegemewa na wala haikutajwa na yeyote katika wasomi wa Hadiyth[2]. Midhali haisihi kuitumia kama dalili hivyo haijuzu. Kwa sababu ´ibaadah hazisihi isipokuwa kwa dalili  za wazi.

c) Kufanya Tawassul kwa dhati ya viumbe haijuzu. Kwa sababu ikiwa “baa” ni ya kiapo basi ni kumuapia Allaah (Ta´ala) na ikiwa kiapo ni kutoka kwa kiumbe kwenda kwa kiumbe basi haitojuzu. Pia isitoshe ni shirki, kama ilivyokuja katika Hadiyth. Tusemeje kuapa kwa kiumbe juu ya Allaah (Jalla wa ´Alaa)? Ikiwa “baa” ni kwa njia ya sababu, basi itambulike kuwa Allaah (Subhaanah) hakufanya kuomba kwa viumbe kuwa ni sababu ya kujibiwa na wala hakuwawekea viumbe Wake jambo hilo katika Shari´ah.

d) Kufanya Tawassul kwa haki za viumbe ni jambo lisilojuzu kwa sababu mbili:

Ya kwanza: Allaah (Subhaanah) hakuna haki ya yeyote ambayo inamlazimu. Yeye (Subhaanah) ndiye amewatunuku viumbe kwa jambo hilo. Amesema (Subhaanah):

وَكَانَ حَقًّا عَلَيْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِينَ

“Ikawa ni haki Kwetu daima kuwanusuru waumini.”[3]

Kule mwenye kumtii kustahiki malipo ni kustahiki kwa njia ya fadhilah na neema na sio kustahiki kwa njia ya nipe nikupe kama inavyokuwa kutoka kwa kiumbe kwenda kwa kiumbe mwengine.

Ya pili: Haki ambayo Allaah amemtunuku mja Wake ni haki maalum kwake yeye na haina mafungamano na mwengine. Mwengine ambaye haiistahiki akifanya Tawassul kwayo basi anakuwa ni mwenye kufanya Tawassul kwa kitu cha kando. Hana mafungamano yoyote nayo, kitu ambacho hakimsaidii kitu.

Kuhusu Hadiyth inayosema:

“Nakuomba kwa haki ya waombaji.”

ni Hadiyth ambayo haikuthibiti. Katika cheni ya wapokezi wake kuna ´Atwaa’ bin al-´Awfiy. Ni mnyonge ambaye kuna maafikiano juu ya unyonge wake, kama walivosema baadhi ya Muhaddithuun. Mambo yakishakuwa hivo basi hatumiwi kama hoja katika masuala haya muhimu miongoni mwa masuala ya ´Aqiydah.

Isitoshe ndani yake hakuna kitu kinachoonyesha kufaa kufanya Tawassul kwa haki ya mtu maalum. Ndani yake kuna kufanya Tawassul kwa haki ya waombaji wote. Haki ya waombaji ni kujibiwa, kama Allaah alivyowaahidi jambo hilo. Hii ni haki ambayo Allaah amejiwabishia Mwenyewe juu yao. Hakuna yeyote aliyemuwajibishia. Ni kufanya Tawassul Kwake kwa ahadi Yake ya kweli na si kwa haki ya kiumbe.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (01/318-319).

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (01/319).

[3] 30:47

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 144-146
  • Imechapishwa: 11/06/2020