Kufanya Tawassul kwa viumbe kumwelekea Allaah

Tawassul ni kujikurubisha kwa kitu. al-Wasiylah maana yake ni kujikurubisha. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَابْتَغُوا إِلَيْهِ الْوَسِيلَةَ

“Tafuteni njia za kumkuruba.”[1]

Bi maana tafuteni kujikurubisha Kwake (Subhaanah) na kufuata radhi Zake. Tawassul imegawanyika aina mbili:

1- Tawassul inayokubalika Kishari´ah. Nayo imegawanyika aina mbalimbali:

Ya kwanza: Ni kufanya Tawassul kwa Allaah (Ta´ala) kwa majina na sifa Zake. Hayo yameamrishwa na Allaah (Ta´ala) pale aliposema:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”Allaah ana majina mazuri mno, hivyo basi muombeni kwayo na waacheni wale wenye kupondoka katika kuyapotosha majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[2]

Ya pili: Kufanya Tawassul kwa Allaah (Ta´ala) kwa imani na matendo mema yaliyofanywa na yule mfanyaji Tawassul. Amesema (Ta´ala) kuhusu waumini:

رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا ۚ رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الْأَبْرَارِ

“Mola wetu, hakika sisi tumemsikia mwenye kunadi akiita katika imani kwamba “mwaminini Mola wenu” ambapo tukaamini.  Mola wetu, tusamehe dhambi zetu na tufutie makosa yetu na tufishe pamoja na waja wema.”[3]

Vilevile kama ilivyopokelewa katika Hadiyth ya wale watu watatu ambao pango liliwafungia ambapo wakajaribu kufungua mlango wa pango hilo lakini hata hivyo hawakuweza kutoka. Matokeo yake wakafanya Tawassul kwa Allaah kwa matendo yao mema[4] ambapo Allaah akawafariji na wakatoka wakitembea.

Ya tatu: Kufanya Tawassul kwa Allaah kwa kumpwekesha kama alivyofanya Yuunus (´alayhis-Salaam):

فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ

“Akaita katika viza kwamba: “Hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe, utakasifu ni Wako.”[5]

Ya nne: Kufanya Tawassul kwa Allaah (Ta´ala) kwa mtu kudhihirisha udhaifu, kumuhitajia na kumdhalilikia Allaah. Ayyuub (´alayhis-Salaam) alisema:

أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ

“Hakika mimi nimepatwa na dhara, Nawe ndiye mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu.”[6]

Ya tano: Kufanya Tawassul kwa Allaah kwa du´aa za waja wema waliohai. Maswahabah pindi walipokuwa wakipatwa na ukame wakimuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awaombee du´aa. Baada ya kufariki walikuwa wakimuomba du´aa ami yake ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) akiwaombea[7].

Ya sita: Kufanya Tawassul kwa Allaah kwa kukiri dhambi:

قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي

“Akasema: “Mola wangu! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu, hivyo basi nisamehe.”[8]

[1] 05:35

[2] 07:180

[3] 03:193

[4] Hayo yamo ndani ya Hadiyth iliopokelewa na al-Bukhaariy (2102) na Muslim (2743) kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[5] 21:87

[6] 21:83

[7] Majmuu´-ul-Fataawaa (01/224) na ”ar-Radd ´alaa al-Bakkriy”, uk. 268.

[8] 28:16

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 143-144
  • Imechapishwa: 11/06/2020