Kuwa na subira na kutarajia malipo kwa Allaah wakati wa msiba

Swali: Sisi wote ni familia na wengi wetu tumehudhuria mkutano huu uliobarikiwa. Tumepata wageni katika nchi hii iliyobarikiwa. Allaah ametukadiria maudhi ya wachawi na waovu katika mashaytwaan kutushambulia na tunamshukuru Allaah kwa kila hali. Hivi sasa tumeanza kufanya matibabu, jambo ambalo ni gumu. Lakini hata hivyo nafsi inachoka na khaswa pindi mtu anapoyaona hayo kutoka kwa mtu ambaye yuko karibu zaidi na yeye. Hakika miongoni  mwa kumkirimu mgeni ni kumliwaza. Hakika ya muislamu kwa muislamu mwenzake ni pamoja na kumuusia kufanya subira. Je, una maneno yoyote ambayo yatatuondoshea msongo wa mawazo, ukuta wa huzuni na giza. Allaah akuondoshee matatizo yako na atusamehe sisi na wazazi wako.

Jibu: Hapana shaka kwamba hali hii iliyotajwa na muulizaji ni yenye kuhuzunisha. Lakini ni juu ya kila mtu ambaye amefikwa na msiba awe na subira. Mtu anatakiwa kutambua kuwa misiba hii inafuta makosa yake. Endapo mtu atatarajia vilevile malipo kutoka kwa Allaah basi Allaah anamnyanyua daraja. Halafu jengine ni kwamba iwapo atasubiri, akalisahau jambo, basi anaweza kupona kwalo. Kwa sababu wasiwasi/mawazo ya ndani ya nafsi yana taathira kwa kuyabakiza na kuyazidisha maradhi. Mtu akiyakataa maradhi haya na akawa si mwenye kuyafikiria, basi kwa idhini ya Allaah atapona. Kwa hivyo nawanasihi muwe na subira, mtarajie malipo kutoka kwa Allaah na msubiri faraja kutoka Kwake:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika amri Yake anapotaka chochote hukiambia: “Kuwa!” nacho huwa.”[1]

Ni watu wangapi ambao walifikia katika kiwango cha kufa lakini hata hivyo roho zao hazikutoka katika miili yao na Allaah akawapona!

[1] 36:82

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (37) http://binothaimeen.net/content/839
  • Imechapishwa: 11/06/2020