77. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya karama za mawalii

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nathibitisha karama za mawalii na mambo ya mukashafati.

MAELEZO

Wakati (Rahimahu Allaah) alipomaliza kutaja ambayo ni wajibu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambayo ni wajibu kwa Maswahabah zake na ambayo ni wajibu kwa watu wa nyumbani kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndipo akahamia kubainisha imani juu ya karama za mawalii.

Karama ni kitu kinatoka nje ya kawaida. Kitu hicho kinatoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) na si kwa mtu. Kikipitika mikononi mwa Mtume inakuwa ni miujiza. Kwa mfano:

– Kukithiri chakula kidogo mikononi mwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoka maji kati ya vidole vyake. Kubwa kuliko yote hayo ni kuteremka Qur-aan ambayo ni miujiza mkubwa wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao umewashinda majini na watu kuleta Suurah mfano wake.

– Bakora ya Muusa, mkono wa Muusa na zile Aayah tisa ambazo Allaah alimpa Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

– Aliyopewa ´Iysaa katika kuwapa uhai wafu, kuwaponyesha vipofu na wenye ukoma.

Hii ni miujiza. Yale aliyopewa Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika miujiza ni mingi sana.

Ama jambo lisilokuwa la kawaida likipitika mikononi mwa mja mwema ambaye si Mtume ni karama kutoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kama mfano wa yaliyokuwa yakipitika kwa Maryam wakati alipojitenga mahali na akajizuia kutokamana na watu na akijiwa na riziki yake akiwa mahali pake:

كُلَّمَا دَخَلَ عَلَيْهَا زَكَرِيَّا الْمِحْرَابَ

“Kila ambapo Zakariyyaa alipoingia kwake katika chumba cha kuswalia… “

Bi maana mahali anaposwalia. Kila pale ambapo Zakariyyaa anaingia mahali pa kuswalia ambapo ni Mihraab:

وَجَدَ عِندَهَا رِزْقًا ۖ قَالَ يَا مَرْيَمُ أَنَّىٰ لَكِ هَـٰذَا ۖ قَالَتْ هُوَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ

“… alikuta kwake kuna riziki. Akasema: “Ee Maryam! Umepata wapi haya?” Akasema: “Haya ni kutoka kwa Allaah. Kwani hakika Allaah anamruzuku amtakaye pasi na hesabu.”[1]

Kadhalika mfano wa yale yaliyopitika kwa watu wa pangoni katika karama kwa sababu walikuwa waumini. Walijitenga na dini ya washirikina, wakatoka nje ya mji na kukimbilia ndani ya pango kwa ajili ya kusalimisha dini yao. Allaah akawapa usingizi kwa miaka mingi mpaka nywele na kucha zao zikawa refu. Kipindi chote hicho walikuwa wakijigeuza upande mmoja kwenda mwingine. Walipitikiwa na miaka mingi bila ya wao kubadilika wakiwa ndani ya usingizi wao. Hizi zilikuwa miongoni mwa karama zao.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah ana kitabu “al-Furqaan bayn Awliyaa´-ir-Rahmaan wa Awliyaa´-ish-Shaytwaan”. Ni kitabu chenye thamani na kizuri sana juu ya maudhui haya.

Lakini mambo haya yasiyokuwa ya kawaida yakipita mikononi mwa mtu kafiri au mchawi sio karama. Ni matendo ya ki-Shaytwaan. Mchawi anaweza kuruka angani, akatembea juu ya maji, akaingia ndani ya moto na usimchome. Haya ni matendo ya ki-Shaytwaan na sio karama. Ni majaribio na mtihani.

Sisi tunaamini karama za mawalii na kwamba ni tunuku kutoka kwa Allaah. Wanachuoni wamesema[2] kuwa karama za mawalii ni miujiza kwa Mitume. Hawakupata karama hizi isipokuwa ni kwa sababu ya kuwafuata Mitume. Kwa hiyo ni karama kwa mawalii na ni miujiza kwa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

[1] 03:37

[2] Tazama ”an-Nubuwwaat”, uk. 130 ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 111-112
  • Imechapishwa: 20/05/2021