Watu wamegawanyika mafungu matatu juu ya karama za mawalii:

1- Wanaopinga karama: Nao ni Mu´tazilah. Wanasema kuwa hakuna karama wala mambo yasiyokuwa ya kawaida. Kwa sababu wanategemea akili zao na hawategemei dalili. Kwa hivyo wanapinga dalili.

2- Waliopindukia katika kuthibitisha karama mpaka wakazingatia matendo ya wachawi, waganga na ya Suufiyyah ni karama. Haya ni matendo ya ki-Shaytwaan na sio karama. Hawa wamechupa mpaka katika kuthibitisha karama mpaka wakaamini kuwa kila kitu kinachokwenda kinyume na ada ni karama ijapokuwa kitu hicho kitafanywa kupitia mikono ya mchawi, mganga na mshirikina. Yote hayo wanazingatia ni karama. Kwa ajili hiyo ndio maana wanayaabudu makaburi na wanasema kuwa mwenye nalo alikuwa na karama na alikuwa na kadhaa na kadhaa na wanaliomba msaada. Huku ni kuchupa mpaka juu ya watu wenye karama.

3- Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambao wanapita kati na kati. Wanathibitisha karama sahihi. Ama matendo ya mashaytwaan na yale yanayopitika mikononi mwa mashaytwaan sio karama. Mambo yalivyo ni kwamba ni ushetani, majaribio na mtihani. Mchawi anaweza kuruka angani, akatembea juu ya maji na akafanya mambo mengi. Lakini haya ni kwa msaada wa mashaytwaan. Vilevile anaweza kuelezea mambo yaliyojificha kwa sababu shaytwaan ndiye kamweleza ikiwa atawaabudu, akawanyenyekea na kuwatumikia:

رَبَّنَا اسْتَمْتَعَ بَعْضُنَا بِبَعْضٍ وَبَلَغْنَا أَجَلَنَا الَّذِي أَجَّلْتَ لَنَا

“Mola wetu! Tulinufaishana baadhi yetu na wengineo na tumefikia muda wetu ambao Umetupangia.”[1]

Mtu akijikurubisha kwa majini ambapo akawanyenyekea ndio wanamtumikia. Wanao uwezo wa mambo yasiyowezwa na watu. Matokeo yake mjinga akafikiria kuwa hizi ni karama ilihali sio karama. Ni ushetani. Ni lazima kuzinduka juu ya mambo haya. Karama hazipingwi moja kwa moja na wala hazithibitishwi moja kwa moja. Ni jambo linatakiwa kupambanuliwa ili mtu awe juu ya utambuzi.

Maneno yake:

“… mambo ya mukashafaat.”

Bi maana farasa. Allaah huwapa baadhi ya waumini farasa ambayo kwayo wanayahisi mambo na yakatokea kama walivyohisi.

[1] 06:128

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 112-113
  • Imechapishwa: 20/05/2021