76. Matamshi ya Tashahhud – Tamko la ´Umar bin al-Khattwaab

5- Tashahhud ya ´Umar bin al-Khattwaab. Alikuwa (Radhiya Allaahu ´anh) akiwafunza watu Tashahhud ilihali amesimama juu ya mimbari akisema:

التحيات لله، الزاكيات لله، الطيبات [لله]، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Maadhimisho yanamstahikia Allaah, matendo mazuri yanamstahikia Allaah na mazuri yote [yanamstahikia Allaah]. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”[1]

[1] Maalik na al-Bayhaqiy ambaye amesahihisha cheni ya wapokezi. Japokuwa Hadiyth imepokelewa kutoka kwa Swahabah ina hukumu moja kama ambavo ingelipokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu kitu kama hicho hakiwezi kusemwa kutokana na maoni ya mtu mwenyewe. Lau kama ingekuwa inahusiana na maoni, basi isingelikuwa na haki zaidi ya kufuatwa kuliko du´aa nyenginezo, kama alivosema Ibn ´Abdil-Barr.

Tanbihi!

Matamshi yote yaliyotajwa hakuna nyongeza:

و مغفرته

“… na msamaha Wake.”

Kwa hiyo mtu asiyazingatie. Kwa ajili hiyo kuna baadhi ya Salaf walioyapinga. at-Twabaraaniy amepokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Twalhah bin Muswrif ambaye amesema:

“Rabiy´ bin Khaytham aliongeza katika Tashahhud:

و بركاته و مغفرته

“… na baraka na msamaha Wake.”

ambapo ´Alqamah akasema: “Unatakiwa kusimama kama tulivyofunzwa:

السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته

“Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume!” (1/56/3)

´Alqamah alijifunza haya kutoka kwa mwalimu wake ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Imepokelewa kwamba kuna mtu mmoja alimfunza Tashahhud. Alipofika:

أشهد أن لا إله إلا الله

“Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah… “

mtu yule akasema:

وحده لا شريك له

“… hali ya kuwa yupekee, hana mshirika… “

Ndipo ´Abdullaah akasema: “Mambo ni hivo kweli, lakini tunasimama pale tulipofunzwa.” (Ameipokea at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Awsatw” (2848) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kuhusu kwamba al-Musayyab al-Kaamiliy aliyasikia haya kutoka kwa Ibn Mas´uud.)

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 142-143
  • Imechapishwa: 01/01/2019