Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nako ni kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitenga mbali na Shirki na watu wake. 

MAELEZO

Neno Uislamu limechukuliwa pindi mtu anapojisalimisha kwenye kitu wakati anapokinyenyekea. Kunasemwa ´ameisalimisha nafsi yake kuuliwa` na kukakusudiwa kwamba amenyenyekea kuuliwa. Mtu anaisalimisha nafsi yake kwenye kitu pindi anapokinyenyekea. Uislamu ni kumsalimishia uso, makusudio na nia Allaah (´Azza wa Jall):

وَمَنْ أَحْسَنُ دِينًا مِّمَّنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلَّـهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ وَاتَّبَعَ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا

“Na nani aliye bora zaidi kwa dini kuliko yule aliyejisalimisha kwa Allaah ilihali ni mtendaji mema na akafuata mila ya Ibraahiym aliyejiengua na shirki na akaelemea Tawhiyd.”[1]

بَلَىٰ مَنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلَّـهِ

“Ndio! Bali yeyote aliyeusalimisha uso wake kwa Allaah.”[2]

Bi maana ameyatakasa matendo Yake kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) na kumnyenyekea Yeye kwa kutaka na kupenda kwake mwenyewe.

Kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd – Ni kule kumpwekesha Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa ´ibaadah. Hii ndio maana ya Tawhiyd. Kwa hiyo yule mwenye kumwabudu Allaah hali ya kuwa yupekee hana mshirika basi amejisalimisha Kwake.

Kunyenyekea Kwake kumtii – Katika yale aliyokuamrisha na akakukataza nayo. Yale aliyokuamrisha, unayafanya, na yale aliyokukataza unayaacha hali ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kujitenga mbali na shirki na watu wake – Kujitenga maana yake ni kukata, kuepuka na kujiweka mbali na shirki na washirikina kwa njia ya kuamini ubatilifu wa shirki na ukajiweka mbali nayo na ukaamini ulazima wa kuwafanyia uadui washirikina kwa sababu wao ni maadui wa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo usiwafanye ni wapenzi. Bali unachotakiwa ni kuwafanya maadui. Kwani wao ni maadui wa Allaah, Mtume Wake na dini Yake. Hivyo usiwapende na usiwafanye ni marafiki. Kinachokupasa ni wewe kuwakata katika dini na ujitenge mbali nao na uamini ubatilifu wa yale waliyomo. Hivyo usiwapende kwa moyo na wala usiwanusuru kwa maneno na vitendo. Kwani wao ni maadui wa Mola Wako na ni maadui wa dini yako. Ni vipi utawafanya kuwa marafiki ilihali ni maadui wa Uislamu?

Haitoshi kwako kwamba unajisalimisha kwa Allaah na unanyenyea Kwake kwa kumtii na wewe hujitengi mbali na shirki na washirikina, jambo hili halitoshi. Wala huzingatiwi kuwa ni muislamu mpaka usifike kwa sifa zifuatazo:

Ya kwanza: Kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd.

Ya pili: Kunyenyekea Kwake kwa kumtii.

Ya tatu: Kujitenga mbali na yanayopingana na Tawhiyd na yanayopingana na utiifu ambayo ni shirki.

Nne: Kujitenga mbali na washirikina.

Kwa kuhakikisha sifa hizi ndio mtu anakuwa muislamu. Ama kukipungua sifa moja tu basi huwi muislamu. Kwa maneno haya matatu ndio Shaykh akafupiza maana ya Uislamu. Ni watu wangapi wasiojua maana ya Uislamu? Hilo si kwa jengine ni kwa sababu hawakujifunza jambo hili. Wakiulizwa nini maana ya Uislamu basi hawawezi kujibu jibu sahihi.

[1] 04:125

[2] 02:112

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 157-159
  • Imechapishwa: 04/01/2021