Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa pili ni kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili. 

MAELEZO

Wakati Shaykh alipomaliza kubainisha msingi wa kwanza, ambao ni kumjua Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa dalili, ndipo akahamia kubainisha msingi wa pili ambao ni kuijua dini ya Uislamu kwa dalili ambapo amesema:

“Msingi wa pili ni kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili.”

Halafu akaiarifisha, kubainisha maana yake na akataja daraja zake ambapo akasema (Rahimahu Allaah):

“Kuijua dini ya Uislamu.”

Makusudio ya dini ni utiifu. Kunasemwa دان له pindi anapomtii katika aliyoamrisha na kuacha aliyokataza.

Wakati mwingine kunasemwa “dini” na kunamaanishwa hesabu pale aliposema:

مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ

“Mfalme wa siku ya malipo.”[1]

Kunasemwa دانه anapofanyiwa hesabu. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ

”Na nini kitakachokujulisha siku ya malipo? Kisha nini kitakachokujulisha siku ya malipo?”[2]

 Bi maana siku ya malipo:

يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

“Siku ambayo nafsi haitokuwa na uwezo wowote juu ya nafsi nyingine na amri siku hiyo ni ya Allaah pekee.”[3]

Kwa dalili – Kuijua dini ya Uislamu hakukuwi kwa kufuata kichwa mchunga na hakukuwi kutoka kwenye kichwa cha mtu. Dini ni lazima iwe kwa mujibu wa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

Kuhusu mtu ambaye haijui dini yake bali yeye anawafuata watu kibubusa na anakwenda kipofu pamoja na watu, basi huyu haijui dini yake na kuna uwezekano mkubwa juu yake:

“Atapoulizwa: “Ni nani Mtume wako?” Atasema: “Sijui. Aah, aah,  sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema.”

 Kwa hiyo ni lazima kwa mtu kuijua dini yake kwa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah, jambo ambalo halifikiwi isipokuwa kwa kusoma.

[1] 01:04

[2] 82:17-18

[3] 82:19

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 155-157
  • Imechapishwa: 04/01/2021