Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye nyoyo na ndimi zilizo salama kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivo ndivo Allaah amewasifia katika maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ

”Na wale waliokuja baada yao ni wenye kusema: “Mola wetu, Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie katika nyoyo zetu mafundo kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.” (59:10)

Wanamtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Msiwatukane Maswahabah zangu! Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Lau mmoja wenu atatoa dhahabu sawa na Uhud, haitofikia kibaba kilichotolewa na mmoja wao wala nusu yake.”[1]

MAELEZO

Mlango huu ni miongoni mwa milango bora na muhimu kabisa ya kitabu hiki ambacho ni “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah” kuhusiana na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Ndani yake mna Radd kwa Raafidhwah na Nawaaswib. Vilevile ndani yake mna ubainifu wa fadhilah na nafasi zao (Radhiya Allaahu ´anhum). Ni mlango mkubwa. Mtunzi wa kitabu amefanya vizuri kabisa kwa kuleta ibara ambazo ziko wazi na bainifu zaidi.

Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah (Radhiya Allaahu ´anhum) ni wenye mioyo na ndimi zilizo salama kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mioyo yao iko salama. Wanawapenda na kuwatakia radhi. Kwa sababu kuwapenda ni sehemu katika dini (Radhiya Allaahu ´anhum). Wao ndio wabebaji wa Shari´ah na karne bora. Kwa ajili hiyo ndio maana kuwapenda ikawa ni dini. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanawapenda kwa ajili ya Allaah na mioyo yao iko salama juu yao. Ni wenye mapenzi tele juu yao. Ndimi zao ziko salama kwa njia ya kwamba hawawatukani na wala hawawatii kasoro. Badala yake wanawatakia radhi na kuwaombea du´aa. Kwa sababu kufanya hivyo ni kumtii Allaah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na waliokuja baada yao wanasema: “Mola Wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa imani wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu chuki kwa walioamini. Mola Wetu! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu!” (49:10)

Isitoshe wanatekeleza wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Msiwatukane Maswahabah zangu! Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Lau mmoja wenu atatoa dhahabu sawa na Uhud, haitofikia kibaba kilichotolewa na mmoja wao wala nusu yake.”

[1] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 111
  • Imechapishwa: 03/11/2024