Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ya wajibu ni mambo nane:

1 – Takbiyr zote mbali na Takbiyrat-ul-Ihraam.

2 – Kusema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

katika Rukuu´.

3 –  Kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

kwa imamu na kwa anayeswali peke yake.

4 – Kusema:

رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ

”Ee Mola Wetu! Ni Zako himdi zote.”

Itasemwa na wote.

5 – Kusema:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika Mola wangu Aliye juu kabisa.”

katika Sujuud.

6 – Kusema:

رَبِّ اغْفِرْ لِي

“Mola! Nisamehe!”

baina ya Sajdah mbili.

7 – Tashahhud  ya kwanza.

8 – Kukaa katika Tashahhud hiyo.

MAELEZO

Maneno yake:

”Ya wajibu ni mambo nane.”

Wakati mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) alipomaliza nguzo za swalah akazungumzia mambo ya wajibu ya swalah.

1 – Takbiyr zote mbali na Takbiyrat-ul-Ihraam.

Takbiyrat-ul-Ihraam sio katika yale mambo ya wajibu ya swalah. Bali ndio nguzo kubwa zaidi katika swalah. Swalah haifungiki isipokuwa kwayo. Takbiyr zote mbali na Takbiyrat-ul-Ihraam. Kama mfano wa Takbiyr ya Rukuu´, Takbiyr ya Sujuud, Takbiyr ya kuinuka kutoka katika Suuud na Takbiyr ya kusimama kutoka katika Tashahhud ya kwanza. Zote hizi zinaingia katika yale mambo ambayo ni ya lazima ndani ya swalah. Ina maana kwamba yule atakayeziacha kwa makusudi swalah yake inabatilika. Lakini mtu akiziacha kwa kusahau ataunga kwa kusujdu sijdah ya kusahau.

2 – Kusema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

katika Rukuu´.

Hili ni jambo la wajibu la pili miongoni mwa yale mambo ya wajibu ya swalah. ´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza: ”Wakati kulipoteremka:

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ

”Basi sabihi kwa jina la Mola wako Mkuu kabisa.”[1]

”Fasabih bismi rabika ladhim”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

”Ijaalieni katika Sujuud zenu.”[2]

 Akiacha kusema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

kwa makusudi, swalah inabatilika. Akiacha kwa kusahau ataiunga kwa sijdah ya kusahau.

Kilicho cha lazima ni yeye kusema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

mara moja, utekelezaji timilifu zaidi ni mara tatu. Endapo atazidisha ndio bora.

3 –  Kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

kwa imamu na kwa anayeswali peke yake.

Hili ni jambo la wajibu la tatu miongoni mwa yale mambo ya wajibu ya swalah. Maana yake ni kwamba Allaah amemuitikia mwenye kumhimidi.

Maamuma hawatakiwi kusema:

سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَه

“Allaah amemsikia mwenye kumhimidi.”

Bali wao watatakiwa kusema:

رَبَّنَا وَ لَكَ الْحَمْدُ

”Ee Mola Wetu! Ni Zako himdi zote.”

Kwa sababu analazimika kusema hivo. Wako wanazuoni wengine wenye kuona kuwa anatakiwa kusema hivo kama imamu[3]. Lakini maoni ya sawa ni kwamba hilo ni maalum kwa imamu na yule anayeswali peke yake.

[1] 56:96

[2] Abu Daawuud (879), Ibn Maajah (887) na Ahmad (04/155).

al-Haakim amesema:

”Hadiyth hii ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh lakini haikupokelewa na al-Bukhaariy na Muslim.” (al-Mustadrak (02/519)).

an-Nawawiy amesema:

”Ameipokea Abu Daawuud na Ibn Maajah kwa cheni ya wapokezi nzuri.” (Khilaaswat-ul-Ahkaam (01/396)).

[3] Tazama ”al-Mughniy” (01/301).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 104-106
  • Imechapishwa: 04/07/2022