74. Kugawanyika kwa watu katika mafungamano yao na Tawhiyd

Watu wanagawanyika katika mafungu yafuatayo:

Fungu la kwanza ni wale wanaoiamini Tawhiyd moyoni mwao na wanatambua ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba kumuabudu mwengine asiyekuwa Yeye ni batili. Lakini hata hivyo hayatendei kazi kwa viungo vyake na wala hayakubali kwa kuyazungumza kutokana na maslahi ya kidunia. Huyu ni kafiri. Ni kama mfano wa Fir´awn. Fir´awn alikuwa akiitambua Tawhiyd moyoni mwake na kwamba yale aliyokuja nayo Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni haki. Lakini aliacha kuitendea kazi na akajidhihirisha kupingana nayo na kuikanusha kwa ajili ya kiburi na ukaidi. Amesema (Ta´ala):

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا ۚ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ

“Wakazikanusha na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha kwa dhulma na majivuno; basi tazama vipi ilikuwa hatima ya mafisadi.” (27:14)

Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Fir´awn:

قَالَ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا أَنزَلَ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ بَصَائِرَ

“Hakika umekwishajua kwamba hakuna Aliyeteremsha haya isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi kuwa ni dalili za kuonekana waziwazi.” (17:102)

Bi maana kwa hakika ulijua ya kwamba hakuna mwengine aliyeteremsha alama hizi nilizokuja nazo isipokuwa ni Mola wa mbingu na ardhi ikiwa ni dalili za wazi kuwaonyesha watu. Hii ni dalili inayothibitisha kuwa Fir´awn alikuwa akiyakinisha ukweli wa yale aliyokuja nayo Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aliyakanusha na akajidhihirisha kuyakanusha kama walivyofanya makafiri wa ki-Quraysh. Allaah amesema juu yao:

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Kwa yakini Tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Basi hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha Aayaat (na ishara) za Allaah.” (06:33)

Aayah inathibitisha kuwa makafiri wa ki-Quraysh wanamsadikisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) moyoni mwao lakini hata hivyo wanayakanusha hayo kwa uinje wao na kwa ndimi zao. Vilevile Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu mayahudi:

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ

“Wale Tuliowapa Kitabu wanamtambua kama wanavyotambua watoto wao.” (02:146)

Wanayatambua haya ndani ya nyoyo zao na wanajidhihirisha kuficha na kukanusha na wakati huo huo wanayayakinisha ndani ya nyoyo zao ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Mtume wa Allaah na kwamba amekuja na haki kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Lakini hakuna kingine kilichowazuia kumfuata isipokuwa ni kiburi na hasadi. Kuamini kwao ndani ya moyo hakuwanufaishi kitu. Ni makafiri wataodumishwa Motoni milele.

Waabudu makaburi wengi hii leo wako namna hii. Utawaona wanasema kuwa wanaelewa na kukubali kwamba yale tunayosema ndio Tawhiyd lakini hata hivyo wanasema kuwa hawako tayari kwenda kinyume na watu wa miji yao kwa kuwa watu wa miji yao wako na makaburi na wanawaomba uokozi maiti na kwamba eti hawawezi kwenda kinyume nao. Lengo ni ili waweze kuishi nao. Aidha wanasema kuwa hawawezi kupambana na watu. Watu hawa ni wenye kuafikiana na washirikina katika ´Aqiydah yao. Ima wafanye kama wanavyofanya wao na wakati huo huo wanaonelea kuwa ni upotevu au wasiwakataze na wala wasibainishe haki. Bali sivyo tu huenda wakafikia mpaka kuwatetea. Huu ndio uhalisia wa mambo hii leo. Wanasema kumwambia ambaye analingania katika haki kwamba ni Khaarijiy na kwamba mtu huyo ameleta madhehebu ya tano. Haya pamoja na kuwa wakati huo huo wanaamini kuwa yale aliyoleta ndio yale yale yaliyoleta Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ndivyo inavyopelekea Qur-aan na Sunnah. Wanayatambua haya. Kilichowapelekea katika hayo ni ima hasadi, kiburi au maslahi ya kidunia. Wanafikiri endapo wataafikiana na haki hii na kuikubali basi watakosa nafasi zao, mali zao na heshima zao mbele za watu.

Fungu la pili ni wale wanaoafiki kidhahiri na wanatamka kwa Tawhiyd na wakakubali kuwa yasemwayo ndio sahihi na ndio haki na wakati huo huo moyoni hawaamini hivo. Bali wanaonelea kuwa yasemwayo ni ukhurafi na kwamba ni kufuata kichwa mchunga mila za zamani. Kwa msemo mwingine hakuyatendea kazi na wala hakuyazungumza hali ya kuyaamini. Bali wameyafanyia kazi na kuyazungumza kwa unafiki. Ni kama hali ya wale wanafiki waliyoko katika tabaka za chini kabisa Motoni kwa kuwa wanasema kwa midomo yao yasiyokuwemo nyoyoni mwao:

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً

“Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba hakika wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah” na Allaah anajua vyema kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo. Wamefanya viapo vyao kuwa ni ngao.” (63:01-02)

Kwa hivyo kwa kufupisha ni kwamba watu wamefungamana na Tawhiyd katika vigawanyo vitatu:

Fungu la kwanza: Ni wale wanaoitambua na kuiamini kwa ndani na wakati huo huo wakaikanusha na kuipinga kwa nje.

Fungu la pili: Ni wale wanaoitamka na kuitendea kazi kwa nje na wakati huo huo wanaipinga na kuikanusha kwa ndani. Hawa ni wanafiki.

Fungu la tatu: Ni wale wanaoiamini kwa ndani na wanaitendea kazi kwa nje na kwa ndani. Hawa ni waumini waliofaulu.

Kuhusu mafungu mawili ya mwanzo ni makafiri waliokula khasara.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 118-119
  • Imechapishwa: 22/04/2017