74. Hivi ndivo unatakiwa uwe msimamo wa muislamu juu ya Maswahabah wa Mtume

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nawapenda Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na (Radhiya Allaahu ´anhum), nataja mazuri yao, nawatakia radhi, nawaombea msamaha, najizuia kutokamana na mabaya yao, nanyamazia yale yaliyopitika kati yao na naitakidi fadhilah zao. Yote hayo kwa ajili ya kutendea kazi maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[1]

MAELEZO

Nawapenda Maswahabah wa Mtume wa Allaah – Bi maana najenga urafiki nao kwa kuwapenda, kuwaheshimu, kuwafuata na kuwaigiliza. Hii ndio maana ya kuwapenda. Tofauti na wapindaji na wapotevu. Katika kilele chao wanaoshika nafasi ya mbele kabisa ni Shiy´ah wanaowatukana Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanawatukana, wanawakufurisha, wanaona kuwa waliwadhulumu watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakachukua uongozi na kuupora na kwamba unawastahikia watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama wanavyowasemea uongo na kuwazulia waislamu. Tofauti vilevile na Khawaarij ambao wanawakufurisha Maswahabah, wanawapiga vita na kuhalalisha damu zao.

Maneno yake:

“Nataja mazuri yao.”

Hili ndio jambo la wajibu kwa muislamu. Anatakiwa kutaja mazuri yao, kuwatakia radhi, kutaja mazuri yao, kuwatakia radhi na aseme “Radhiya Allaahu ´anhum”. Kila mmoja anapotajwa aseme “Radhiya Allaahu ´anh” (Allaah amuie radhi). Kwa sababu Allaah amesema:

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ

“Hakika Allaah amewawia radhi waumini waliokupa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti.”[2]

Allaah amewawia radhi nao wamemuie radhi.

Anatakiwa kuwatakia radhi, kuwasifia, asimpunguze yeyote katika wao, kutafuta na kuyaanika makosa yao. Hayo yanafanywa na watu waliopinda, waliopotea au wajinga wanaosema kuwa eti wanatafiti historia, eti wanataka kuhakikisha mambo ya kihistoria na wanawakagua Maswahabah na yaliyopitika kati yao kipindi cha fitina. Hiki ni kitu kilichopita. Si wao wenyewe waliochagua fitina. Lakini ilitokea jambo ambalo Allaah alikuwa amekwishalipanga na ndio maana ikatokea fitina na wakapewa majaribio kwayo. Haya yalipitika pasi na kutaka kwao (Radhiya Allaahu ´anhum). Walikuwa wanataka kheri. Walichokuwa wanataka ni kuinusuru dini na wakajitahidi katika jambo hili. Kwa hiyo sisi hatuingii katika jambo hili. Ikibidi kuingia ndani basi tunawatakia udhuru.

Maneno yake:

“Nawaombea msamaha.”

Kwa kutendea kazi Qur-aan. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا ٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini.”[3]

Alipowataja Muhaajiruun na Answaar akasema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani.”

Huu ndio msimamo wa muislamu juu ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Maneno yake:

“Najizuia kutokamana na mabaya yao.”

Sitafuti makosa yao na kufukua mambo yaliyosemwa. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Waasitwiyyah”:

“Kati ya mapokezi haya yaliyopokelewa kuna ambayo ni ya uongo, na kuna ambayo yamezidishwa juu yake na kupunguzwa, na kuna ambayo yamebadilishwa kwa sura yake ya kihakika na ndani yake kuna ya sahihi ambayo wamepewa udhuru kwayo. Ima walikuwa ni wenye kujitahidi baada ya kuifikia haki wakapatia ambapo wanalipwa ujira mara mbili, au walikuwa ni wenye kujitahidi baada ya kuifikia haki wakakosea ambapo wanalipwa ujira mara moja.”[4]

Wao ni wenye kulipwa ujira kwa kila hali. Isitoshe wao wana fadhilah ambazo zinafunika yale makosa yanayoweza kutokea kutoka kwa mmojammoja katika wao. Usuhuba unafunika yote haya.

Kuhusu yaliyotokea kati yao kipindi cha fitina si kwa kutaka kwao wenyewe. Walipewa mtihani kwa sababu ya walinganizi wapotevu ambao walipandikizwa kati yao. Kama mfano wa ´Abdullaah bin Sabaa´ na wale waliomfuata. Matokeo yake wakawa wanaeneza fitina mpaka kukatokea vita. Fitina ya kwanza ilikuwa ni kumponda mtawala. ´Uthmaan alitukanwa na kupondwa. Jambo likaishilia kuuliwa kwa ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh). Alipouliwa ndipo kukafunguka mlango wa mauwaji na wa fitina. Hili ni jambo lililopita juu yao (Radhiya Allaahu ´anhum) na wakapewa mtihani kwalo. Kwa hiyo hatuingii ndani ya yaliyopitika baina yao ambapo tukamtia makosani ´Aliy au tukamtia makosani Mu´aawiyah. Hatuingii baina yao kuhusu jambo hili kabisa kabisa. Yote haya yalitokana na Ijtihaad. Kila mmoja alilenga kuinusuru haki.

Maneno yake:

“Naitakidi fadhilah zao.”

Tunaamini kuwa wao ndio wabora wa Ummah. Hii ni imani ambayo ni ya lazima. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[5]

Vifundo ni chuki na bughudha. Kifuani au moyoni mwako kusiwe na bughudha au chuki kwa yeyote katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 59:10

[2] 48:18

[3] 59:10

[4] Uk. 44.

[5] 59:10

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 106-107
  • Imechapishwa: 19/05/2021