Maswahabah wanashindana ubora. Wabora ni wale makhaliyfah waongofu; Abu Bakr, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan, kisha ´Aliy halafu wale wengine kumi walioshuhudiwa Pepo: Twalhah, az-Zubayr, Sa´d bin Abiy Waqqaas, Sa´iyd bin Zayd, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf na Abu ´Ubaydah ´Aamir bin al-Jarraah. Hawa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewashuhudilia Pepo na amekufa akiwa ni mwenye radhi juu yao – Allaah amewawia radhi nao wamemuia radhi.

Halafu wale waliopigana vita vya Badr ni bora kuliko wengine. Kwa sababu Allaah alizitazama nyoyo zao na akasema:

“Fanyeni mkitakacho nimekwishakusameheni.”[1]

Halafu wale waliokula kiapo chini ya mti – katika sulhu ya Hudaybiyah – wale ambao walitoa kiapo cha usikivu chini ya mti. Amesema (Ta´ala):

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ

“Hakika Allaah amewawia radhi waumini waliokupa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti. Alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao. Basi Akawateremshia utulivu na akawalipa ushindi wa karibu.”[2]

Ameeleza (Subhaanah) kwamba amewaridhia na hivyo akawatunuku radhi Zake.

Halafu Muhaajiruun ni bora kuliko Answaar. Kwa ajili hiyo ndio maana Muhaajiruun wanaanza kutajwa mbele ya Answaar. Amesema (Ta´ala):

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ

“Wale waliotangulia awali miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar.”[3]

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ

“Wapatiwe pia mafuqara Muhaajiruun ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na mali zao.”[4]

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ

“Na wale waliokuwa na makazi [Madiynah]… “

Bi maana Answaar. Siku zote Muhaajiruun hutajwa mwanzo kabla ya Answaar. Wao ndio bora. Si kwa jengine ni kwa sababu wameiacha miji yao, mali zao na watoto wao na wakatoka kwa ajili ya kumnusuru Allaah na Mtume Wake:

وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“… na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake.”

Allaah amewasifia ukweli. Kwa hiyo wanashindana – Allaah amewawia radhi nao wamemuia radhi.

Aliyesilimu kabla ya kufunguliwa mji wa Makkah ni bora kuliko aliyesilimu mwaka wa kufunguliwa mji wa Makkah au baada yake. Amesema (Ta´ala):

لَا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ

“Halingani sawa miongoni mwenu aliyejitolea kabla ya u shindi [wa ufunguzi wa mi wa Makkah] na akapigana.”[5]

Wale waliosilimu kabla ya kufunguliwa mji wa Makkah ni bora kuliko wale waliosilimu baada ya kufunguliwa mji wa Makkah. Lakini wote wanashirikiana katika kusuhubiana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni fadhilah za kijumla. Lakini wanashindana ubora kati yao.

Maneno yake:

“Na kwamba mbora wa Ummah wake ni Abu Bakr as-Swiddiyq.”

Kwa sababu ndiye wa kwanza katika wale makhaliyfah waongofu. Jengine yeye ndiye ambaye Maswahabah walimpa kiapo cha usikivu baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakamchagua kwa sababu walikuwa wanaona yeye ndiye mbora wao.

Maneno yake:

“Kisha ´Umar al-Faaruuq.”

Kwa sababu yeye ndiye alikuwa khaliyfah baada ya Abu Bakr. Abu Bakr alimchagua na kumkabidhi. Hii ni dalili ya kwamba yeye ndiye mbora wa Ummah baada ya Abu Bakr.

Maneno yake:

“Kisha ´Uthmaan.”

Yeye ni watatu. Kwa sababu watu sita wa mashauriano ambao aliwachagua ´Umar walimchagua ´Uthmaan. (Radhiya Allaahu ´anh) kwa sababu ya ubora na nafasi yake.

Maneno yake:

“Halafu ´Aliy al-Murtadhwaa.”

´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ni mtoto wa ami yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mke wake na baba yake na al-Hasan na al-Husayn. Miongoni mwa fadhilah zake ni kwamba yeye:

“Anampenda Allaah na Mtume Wake na Allaah na Mtume Wake wanampenda.”[6]

Hivo ndivo alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ana fadhilah kubwa (Radhiya Allaahu ´anhum). Hii ndio maana ya maneno ya Shaykh.

Maneno yake:

“Kisha wale kumi waliobakia.”

Bi maana wale kumi waliobashiriwa Pepo.

Maneno yake:

“Halafu waliopigana vita vya Badr.”

“Kwa sababu Allaah aliwatazama na akasema:

“Fanyeni mkitakacho nimekwishakusameheni.”[7]

Maneno yake:

“Kisha waliokula kiapo chini ya mti.”

Ambao walimpa ahadi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) chini ya mti juu ya mapambano. Walimpa ahadi juu ya kifo pindi washirikina walipomzuia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake kuingia Makkah kufanya ´Umrah. Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtuma ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) kufanya nao mazungumzo. Kukaja uvumi kuwa ´Uthmaan ameuliwa. Hapo ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaazimia kupambana nao. Akawataka Maswahabah kula kiapo. Walikuwa 1400. Walimpa ahadi ya kifo. Baadaye ikaja kubainika kwamba ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) hakuuliwa. Kisha kukatokea sulhu kati ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wa Makkah kama inavyotambulika. Kinacholengwa ni kwamba Allaah ametaja bay´ah hii, akawasifia watu wake na akawaridhia.

Maneno yake:

“Halafu Maswahabah wengine waliobakia.”

Kwa sababu wanashirikiana katika usuhuba. Wote ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao. Hakuna yeyote anayelingana nao.

[1] al-Bukhaariy (3007) na Muslim (2494) kupitia kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] 48:18

[3] 09:100

[4] 59:08

[5] 57:10

[6] al-Bukhaariy (2975) na Muslim (2407).

[7] al-Bukhaariy (3007) na Muslim (2494) kupitia kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 103-105
  • Imechapishwa: 19/05/2021