73. Dalili kwamba kuchinja ni ´ibaadah na aina na hukumu za vichinjwa mbalimbali

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kuchinja ni Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

“Sema: “Hakika swalah yangu, kichinjwa changu, uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hali ya kuwa hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza.”[1]

na katika Sunnah:

“Allaah Amemlaani yule mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah.”[2]

MAELEZO

 Kuna vichinjwa aina nne:

1- Kuchinja kwa njia ya kujikurubisha na kumuadhimisha mtu. Aina hii haijuzu isipokuwa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa sababu ni miongoni mwa ´ibaadah kuu. Haijuzu kuwachinjia majini, mashaytwaan, wafalme na maraisi kwa lengo la kuwaadhimisha. Kwa sababu hii ni ´ibaadah na ´ibaadah haijuzu kuelekezewa mwengine asiyekuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Wale wanaowachinjia majini kwa ajili ya kusalimika kutokamana na shari zao au kwa ajili ya kumponya mgonjwa, kama wanavofanya waganga na wanajimu ambao wanadai matibabu na wanawaambia watu wachinje kichinjwa fulani ili wawaponye wagonjwa wao na kwamba wasitaje jina la Allaah juu yake ni shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya dini. Haya ndio aliyokusudia Allaah (Ta´ala) hali ya kuwa ni mwenye kutahadharisha watu kumfanyia asiyekuwa Yeye:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

”Sema: “Hakika swalah yangu na kichinjwa changu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee.”[3]

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali kwa ajili ya Mola wako na [pia ukichinja] na chinja [kwa ajili Yake]!”[4]

Bi maana mchinjie Mola wako.

2- Kuchinja kwa ajili ya kula nyama. Aina hii hakina ubaya. Kwa sababu hakuchinja kwa ajili ya kujikurubisha na kumuadhimisha mtu. Amechinja kwa haja na kula. Kichinjwa aina hii haina neno. Kwa sababu sio aina ya ´ibaadah. Vilevile inafaa kuchinja kwa ajili ya nyama.

3- Kuchinja kwa ajili ya furaha kwa mnasaba wa ndoa, kuhamia nyumba mpya, kufika kwa aliyekuwa mbali na mfano wa hayo kwa njia kuwakusanya ndugu. Inafaa vilevile kuchinja kwa lengo la kuonyesha furaha kutokana na kitu alichopata mtu. Aina hii inafaa. Kwa sababu ndani yake hamna kumuadhimisha wala kujikurubisha kwa mtu. Ni kwa lengo la kuonyesha furaha kwa kitu alichopata mtu.

4- Kuchinja kwa ajili ya kutoa swadaqah kuwapa nyama mafukara, masikini na wahitaji. Hii inazingatiwa ni Sunnah na ni jambo linaingia katika ´ibaadah.

[1] 06:162-163

[2] Muslim (1978).

[3] 06:162

[4] 108:02

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 152-154
  • Imechapishwa: 31/12/2020