72. Baadhi ya Adhkaar katika Tashahhud ya mwisho

Miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa ya kimaneno na yale aliyopokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakati mmoja wenu anapomaliza Tashahhud, basi amuombe Allaah ulinzi kutokamana na mambo mane kwa kusema:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ جهنم و من عَذَابِ الْقَبْر ومِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ وَ مِنْ شر فتنة الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba ulinzi kutokamana na adabu ya Jahannam na kutokamana na adhabu ya kaburi, kutokamana na fitina ya uhai na kifo na kutokamana na fitina ya al-Masiyh ad-Dajjaal.”[1]

Hii ni du´aa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha iombwe mwishoni mwa swalah zao. Ummah umeafikiana juu ya kwamba ni jambo limewekwa katika Shari´ah ambalo Allaah na Mtume Wake wanalipenda na kuliridhia. Wakazozana juu ya ulazima wake. Twawuus[2] na baadhi ya wengine wameonelea kuwa ni lazima. Pia ni moja ya maoni katika madhehebu ya Ahmad. Wengi wao wamesema kuwa imependekezwa[3].

Vilevile imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesema kumwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Nifunze du´aa nitayoomba mwishoni mwa swalah yangu?” Akamwambia: “Sema:

اللّهُـمَّ إِنِّـي ظَلَـمْتُ نَفْسـي ظُلْمـاً كَثـيراً وَلا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْت، فَاغْـفِر لي مَغْـفِرَةً مِنْ عِنْـدِك وَارْحَمْـني إِنَّكَ أَنْتَ الغَـفورُ الرَّحـيم

”Ee Allaah! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu dhulma nyingi na hakuna asamehaye dhambi isipokuwa Wewe. Hivyo basi, nisamehe msamaha kutoka Kwako na unirehemu. Kwani hakika Wewe ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[4]

Imepokelewa vilevile katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy kupitia kwa ´Amr bin Maymuun al-Awdiy ambaye amesema: “Sa´d alikuwa akiwafunza wana wake maneno haya  kama mwanafunzi anavyowafunza watoto kuandika na akisema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba ulinzi kutokamana nayo mwishoni mwa swalah:

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَعوذُ بِكَ مِنَ البُخْـل، وَأَعوذُ بِكَ مِنَ الجُـبْن، وَأَعوذُ بِكَ مِنْ أَنْ أُرَدَّ إِلى أَرْذَلِ الـعُمُر، وَأَعوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَـةِ الدُّنْـيا وَعَـذابِ القَـبْر

”Ee Allaah najikinga Kwako kutokamana na ubakhili, najikinga Kwako kutokamana na woga, najikinga Kwako kutokamana na kurudishwa katika umri duni, najikinga Kwako kutokamana na fitina ya dunia na adhabu ya kaburi.”[5]

Zote hizi zimependekezwa.

Tashahhud inamalizika pale unaposema:

اللهم صل على محمد

“Ee Allaah! Msifu Muhammad.“

Lakini timilifu zaidi mtu akamilishe:

و على آل محمد كما صليت على إبراهيم و على آل إبراهيم

“Na jamaa zake Muhammad kama Ulivyomsifu Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym.”

Aombe kinga kwa Allaah kutokamana na mambo mane na aseme:

رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ

“Mola wetu Tupe katika dunia mema na katika Aakhirah pia Tupe mema na tukinge na adhabu ya Moto.”[6]

Akifanya hii ndio du´aa ya mwisho ni jambo limependekezwa. Haitakikani kwa mtu kuacha mambo ya fadhilah.

[1] al-Bukhaariy (1377) na Muslim (588).

[2] Muslim amepokea katika ”as-Swahiyh” yake hali ya kufikiwa bila cheni ya wapokezi akasema:

”Nimefikiwa na khabari kwamba Twawuus alisema kumwambia mwanae: ”Umeiomba ndani ya swalah yako?” Akajibu: ”Hapana.” Akasema: ”Urudie swalah yako.”

[3] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/713).

[4] al-Bukhaariy (734) na Muslim (2705).

[5] al-Bukhaariy (2822).

[6] 02:201

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 103-104
  • Imechapishwa: 30/06/2022