72. Twahara juu ya Sujuud ya kisomo na baadhi ya Adhkaar zinazosomwa

Swali 72: Je, Sujuud ya kisomo inashurutisha mtu kuwa na twahara? Je, aseme “Allaahu Akbar” wakati anapoenda chini na kuinuka ni mamoja mtu yuko ndani ya swalah au nje yake? Kipi kinachosemwa katika Sujuud hii? Je, zimesihi du´aa zilizopokelewa ndani yake? Je, imesuniwa kutoa salamu kutoka katika Sujuud hii akiwa mtu nje ya swalah?

Jibu: Sujuud ya kisomo haishurutishi twahara kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Ndani yake hakuna Tasliym wala Takbiyr wakati wa kuinuka kutoka katika Sujuud hiyo kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Imesuniwa kuleta Takbiyr wakati wa kusujudu. Katika Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) imethibiti yanayofahamisha juu ya hilo.

Lakini ikiwa Sujuud ya kisomo ni ndani ya swalah basi ni lazima kuleta Takbiyr wakati wa kwenda chini na wakati wa kuinuka. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya hivo ndani ya swalah katika kila kupomoka na kila kuinuka. Imesihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah wakati wa Sujuud ya kisomo kuleta Dhikr na du´aa yale yaliyowekwa katika Sujuud ya swalah kutokana na kuenea kwa Hadiyth. Miongoni mwa du´aa hizo ni pamoja na:

اللهم لك سجدت وبك آمنت ولك أسلمت، سجد وجهي للذي خلقه وصوره وشق سمعه وبصره تبارك الله أحسن الخالقين

“Ee Allaah! Kwako nimesujudu, Wewe nimekuamini, Kwako nimejisalimisha, uso wangu umemsujudia Yule ambaye kaumba, akautia sura na akapasua usikizi wake na uoni wake kwa uwezo na nguvu Zake. ametakasika Allaah, mbora wa waumbaji.”

Ameyapokea hayo Muslim katika “as-Swahiyh” yake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa anasema Dhikr hii katika Sujuud ya swalah kutoka katika Hadiyth ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

Punde kidogo imetangulia kuwa imesuniwa katika Sujuud ya kisomo yale yaliyosuniwa katika Sujuud ya swalah. Vilevile imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba aliomba du´aa katika Sujuud ya kisomo kwa kusema:

اللهم اكتب لي بها عندك أجرا وامح عني بها وزرا واجعلها لي عندك ذخرا وتقبلها مني كما تقبلتها من عبدك داود عليه السلام

“Ee Allaah! Niandikie kwayo huko Kwako ujira, nifutie kwayo madhambi, ifanye kwa ajili yangu huko Kwako hazina na ikubali kutoka kwangu kama ulivyoikubali kutoka kwa mja Wako Daawuud (´alayhis-Salaam).”

Ni wajibu kusema:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika Mola wangu Aliye juu.”

kama ilivyo wajibu katika Sujuud ya swalah. Dhikr na du´aa zenye kuzidi hapo zimependekezwa.

Sujuud ya kisomo ndani ya swalah na nje yake ni kitu kimependekezwa na sio lazima. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika Hadiyth ya Zayd bin Thaabit yanayojulisha jambo hilo. Vilevile kumethibiti pia kutoka kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) yanayofahamisha jambo hilo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 76
  • Imechapishwa: 19/09/2022