72. Nguo anayotoka nayo mwanamke isiyoingia akilini

Sharti ya pili ni kuwa jilbaab yenyewe kama yenyewe isiwe yenye mapambo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika… ”[1]

Kuenea kwa Aayah kunakusanya lile vazi la mwanamke analovaa juu ikiwa linavutia macho ya wanamme kumtazama. Hayo yanashuhudiwa na maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ

“Na tulizeni majumbani mwenu na wala msijishauwe mshauwo wa wanawake majahili wa awali.”[2]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Usiulize juu ya watu sampuli tatu[3]: Mwanamme ambaye amejitenga na mkusanyiko, akamuasi kiongozi wake na akafa hali ya kuwa ni muasi, mtumwa au kijakazi ambaye amemkimbia mmiliki wake na mwanamke ambaye mume wake yuko mbali naye na amemtosheleza mahitaji yake ya kidunia kisha akajishaua akitanga huku na huku kuonyesha mapambo yake wakati yuko mbali.”[4]

Kujishaua (التبرج) maana yake ni mwanamke kuonyesha mapambo yake, urembo wake na yale yanayomlazimu kuyafunika na yanayoamsha matamanio ya wanamme[5]. Lengo la kuamrishwa jilbaab ni kwa sababu ya kuficha mapambo ya mwanamke. Kwa hivyo ni jambo lisiloingia akilini jilbaab yenyewe anayovaa ikawa na mapambo.

[1] 24:31

[2] 33:33

[3] Kwa sababu ni wenye kuangamia.

[4] al-Haakim na Ahmad kupitia kwa Fadhwaalah bin ´Ubayd. Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh. as-Suyuutwiy ameiegemeza katika ”al-Jaamiy´” yake al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad”, Abu Ya´laa, at-Twabaaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” na al-Bayhaqiy katika ”Shu´b-ul-Iymaan”. al-Haakim amesema:

”Iko kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Kutokana na ninavojua haina kasoro.”

adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Ibn ´Asaakir amesema kuwa ni nzuri katika ”Madh-ut-Tawaadhu´”.

[5] Imekuja namna hii katika ”Fath-ul-Bayaan” (7/274). Kisha akasema:

”Maoni mengine yamesema ni kule kutembea kwa mtindo, kuyumbayumba na kujivunjavunja. Maoni haya ni dhaifu sana na yale ya kwanza ndio bora.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 119-120
  • Imechapishwa: 10/10/2023