70. Tamko bora na lililokusanya zaidi la kumswalia Mtume

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

اللهم صل على محمد و على آل محمد كما صليت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

”Ee Allaah! Msifu Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyomsifu Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhimidiwa na Mwenye kutukuzwa.”

Allaah kumswalia mja Wake ni kule kumsifu katika ulimwengu wa juu. Kama alivyosema al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kutoka kwa Abul-´Aaliyah aliyesema:

“Allaah kumswalia mja Wake ni kule kumsifu katika ulimwengu wa juu.”

Imesemekana vilevile kwamba ni rehema, lakini ya kwanza ndio sahihi zaidi.

Ama kuhusiana na kwamba Malaika pia wanafanya hivyo, maana yake ni kwamba wanamwombea msamaha, na kwamba wanaadamu wanafanya hivyo, maana yake ni du´aa. Ama kuhusu:

اللهم بارك على محمد و على آل محمد كما باركت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

”Ee Allaah! Mbariki Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhimidiwa na Mwenye kutukuzwa.”

na yanayokuja baada yake, yanazingatiwa kuwa ni katika maneno na matendo yaliyopendekezwa.

MAELEZO

Unamwomba Allaah (Ta´ala) amswalie Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Tazama mpangilio huu wa ajabu. Mosi kunaanza haki ya Allaah ambayo ni yale maadhimisho na swalah. Kisha kunafuatia kumtolea salamu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumwombea du´aa. Kisha unajiombea du´aa mwenyewe na kila mja mwema mbinguni na ardhini. Halafu unamshuhudilia Allaah Umoja. Kisha unamshuhudilia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Ujumbe. Halafu unamswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mpangilio huu ni kwa njia ya kukomeka na haifai kwako kutanguliza au kuchelewesha.

Swahiyh zaidi yaliyopokelewa katika kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kukusanya kati ya Muhammad na jamaa zake Muhammad na kukusanya kati ya Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym katika kumswalia na kumtakia baraka. al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Laylaa ambaye amesema: “Tulikutana na Ka´b bin ´Ujrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye akasema: “Je, nisikupe zawadi niliyoisikia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Nikasema: “Ndio, nipe zawadi.” Akasema: “Tulimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mnaswaliwa vipi, watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani hakika Allaah ametufunza ni namna gani tukutakieni amani?” Akasema: “Semeni:

اللهم صل على محمد و على آل محمد كما صليت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد. اللهم بارك على محمد و على آل محمد كما باركت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

“Ee Allaah! Msifu Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyomsifu Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa. Ee Allaah! Mbariki Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa.”[1]

Hii ndio Swahiyh zaidi, iliyokusanya na bora zaidi.

Haya yamefichikana kwa baadhi ya maimamu wakubwa kama vile Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah[2] na Ibn-ul-Qayyim[3] (Rahimahumaa Allaah) wakasema:

“Hakukupokelewa kukusanya kati ya Muhammad na jamaa zake Muhammad na Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym katika kuswalia na kuwaombea baraka.”

[1] al-Bukhaariy (3370).

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (22/456-457).

[3] Jalaa´-ul-Afhaam (01/292).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 100-102
  • Imechapishwa: 30/06/2022