68. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya Mtume

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naamini kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwisho wa Manabii na Mitume. Imani ya mja haisihi mpaka aamini Ujumbe wake na ashuhudie unabii wake.

MAELEZO

 Wakati (Rahimahu Allaah) mwanzoni mwa kitabu alipotaka baadhi ya misingi ya ´Aqiydah aliyoulizwa ndipo hapa akataja imani yake juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu msingi wa kwanza wa ´Aqiydah ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah ndani yake kunaingia yale yote yanayohusiana na Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) katika Tawhiyd Yake kwa mafungu yake matatu, yale yanayohusiana na matendo Yake, maneno Yake na yale yote yanayohusiana na Mola (Subhaanahu wa Ta´ala). Yote haya yanaingia katika Kuhushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.

Kisha kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Nako ni kule kuthibitisha na kukubali ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtu anatakiwa aliamini hilo kwa moyo wake, alitamke kwa mdomo wake na alifuatizie kwa kumfuata (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kumtii, kutekeleza amri zake na kujiepusha na makatazo yake na kusadikisha khabari zake. Yote haya yanaingia katika kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.

Kunaingia pia kuamini ujumbe wake kuwa umeenea kwa watu na majini wote. Kunaingia vilevile kuamini kwamba yeye ndiye Nabii wa mwisho na kwamba hakuna Nabii mwingine baada yake. Yote haya yanaingia katika kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Ni lazima kwa mtu akubali kwa moyo na atamke kwa ulimi. Haitoshi kutamka kwa ulimi bila ya kutambua kuwa ni Mtume wa Allaah. Wanafiki wanakiri kwamba ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa midomo yao:

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ

”Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah.” – na Allaah anajua vyema kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo.”[1]

ilihali ni waongo katika ushuhuda wao.

Jengine ni kwamba haitoshi kuamini ndani ya moyo bila ya kutamka na kubainisha kwa mdomo. Washirikina walikuwa wakishuhudia ya kwamba ni Mtume wa Allaah kwa mioyo yao. Lakini hawatamki hilo. Walikataa kwa kiburi, ukaidi na ukanushaji kutamka ujumbe wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja na kwamba mioyo yao inakiri jamob hilo. Amesema (Ta´ala):

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”[2]

Mayahudi na manaswara walitambua ya kwamba yeye ni Mtume wa Allaah. Lakini kiburi na hasadi ndivo vilivyowazuia kutamka jambo hilo na kumfuata. Amesema (Ta´ala):

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنْهُمْ لَيَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ ۖ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ

“Wale ambao tumewapa Kitabu wanamjua kama wanavyowajua watoto wao; na hakika kundi miongoni mwao wanaficha haki ilihali wao wanajua. Haki kutoka kwa Mola wako, hivyo basi kamwe usiwe miongoni mwa wenye shaka.”[3]

[1] 63:01

[2] 06:33

[3] 02:146-147

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 98-99
  • Imechapishwa: 17/05/2021