67. Waumini siku ya Qiyaamah watamuona Mola wao kwa macho yao

Maneno yake:

“Waumini watamuona Mola wao kwa macho yao… “

kuna Radd kwa wale wanaosema kuwa watamuona kwa mioyo yao. Kwa sababu kuona kunaweza kuwa kimoyo na kimacho. Wao wanasema kuwa watamuona kwa mioyo yao. Ingelikuwa kwa mioyo yao basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingelisema:

“… kama wanavyouona mwezi usiku wenye mwezi mng´aro na kama wanavyoona mwezi waziwazi pasi na mawingu.”[1]

Je, jua linaonekana kwa moyo au kwa macho? Kwa macho.

Maneno yake:

“… kama wanavyouona mwezi usiku wenye mwezi mng´aro.”

Kama wanavyoona mwezi pindi umetimia katika usiku wa tarehe kumi na tano. Kwa sababu mwezi unakamilika usiku wa tarehe kumi na nne na usiku wa tarehe kumi na tano. Kwa ajili hii zinaitwa “nyusiku ambazo mwezi umetimia.” Wewe unauona waziwazi na watu wengine wote wanauona usiku wa mwezi mng´aro waziwazi. Watu wote ulimwenguni wanauona waziwazi. Hakuna ubishi wowote kwamba watu huuona mwezi kila siku.

Maneno yake:

“Hawatosongamana katika kumtazama.”

Bi maana kila mmoja atamuona kwa urahisi bila ya msongamano wala khatari yoyote. Kwa sababu wakati fulani huenda watu wakasongamana juu ya kitu kimoja na sehemu hiyo kukatokea khatari, kifo au kushindwa. Lakini watamuona Mola wao bila ya kuvutana wala msongamano. Jambo hili linapatikana hata kati ya viumbe ambao wote wanaona mwezi na hawasongamani juu ya kuuona. Vilevile wanaliona jua na hawasongamani katika kuliona. Hali ikiwa namna hii juu ya viumbe, basi kwa Allaah ni jambo lina haki zaidi.

[1] al-Bukhaariy (806, 6573, 7437) na Muslim (182) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Vilevile al-Bukhaariy ameipokea (7439) na Muslim (183) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 96-97
  • Imechapishwa: 17/05/2021