Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ibn Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Twaaghuut ni kila chenye kuabudiwa, kinachofuatwa au kutiiwa ambacho mja anapindukia mipaka yake.”[1]

Twawaaghiyt ni wengi. Wakubwa wao ni watano:

1 – Ibliys, Allaah amlaani.

2 – Yule mwenye kuabudiwa hali ya kuwa yuko radhi kwa hilo.

3 – Yule mwenye kuwaita watu katika kumuabudu.

4 – Yule mwenye kudai kujua kitu katika elimu ya ghaibu.

5 – Yule asiyehukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah.

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ ۚ فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Hapana kulazimisha katika dini, kwani imekwishabainika kati ya Uongofu na upotofu. Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika, na Allaah ni Mwenye kusikia, Mjuzi wa yote.”[2]

MAELEZO

Mpaka wa kila kiumbe ni yeye awe mja wa Allaah. Akivuka mpaka wake na akaridhika kuabudiwa anakuwa  Twaaghuut. Kadhalika mwenye kufuatwa akiridhika kufuatwa katika batili basi amevuka mpaka wake na hivyo anakuwa Twaaghuut. Vivyo hivyo kiumbe akiridhia kutiiwa katika maasi anakuwa Twaaghuut. Mpaka wa kila kiumbe ni yeye kuwa mwenye kumuamini Allaah, mwenye kumtii Allaah, mja wa Allaah na mwenye kufuata njia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

” Twawaaghiyt ni wengi. Wakubwa wao ni watano… ”

Ibliys – Allaah amlaani – ndiye wa kwanza. Yeye ndiye kiongozi wa kila shari na kila fitina.

Anayeabudiwa akiwa radhi. Kwa maana nyingine watu wanamwabudu na huku akiridhia.

Maneno yake mtunzi:

”Dalili ni maneno Yake (Ta´ala).”

Dalili ya kwamba ni lazima kwa mtu kukufuru Twaaghuut na kumuamini Allaah.

Maneno Yake (Ta´ala):

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ

“Hapana kulazimisha katika dini.”

Imesemwa kwamba hili ni kabla ya Shari´ah ya jihaad. Maoni mengine yanasema kuwa Aayah hii imeteremka kuhusu watu wa Kitabu kwa sababu wao wamepewa khiyari ya kuingia katika Uislamu au kulipa kodi.

Uongofu (الرشد) ni dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Upotofu (الغي) ni ukafiri. Kwa maana nyingine uwazi wa imani kutokana na ukafiri.

Kishikilio madhubuti (العروة الوثقى) ni neno la Tawhiyd. Kwa maana nyingine imekwishabainika uongofu kutokamana na upotofu na imani kutokamana na ukafiri. Hakuna yeyote anayetakiwa kulazimishwa kuingia katika dini kwa sababu uongofu umekwishabainika na kuwa wazi. Anayekufuru Twaaghuut basi anatakiwa kujitenga mbali kutokamana na kumwabudu asiyekuwa Allaah, kuyaepuka, kuyachukia, kuyafanyia uadui na kuwafanyia uadui vilevile watu wake. Sambamba na hilo anatakiwa kumuamini Allaah. Huyu ndiye muumini. Kwa msemo mwingine ameshikilia kishikilio madhubuti na hiyo ndio maana ya (لا إله إلا الله).

[1] Tazama ”I´laam-ul-Muwaqqi´iyn” (01/40).

[2] 02:256

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 109-110
  • Imechapishwa: 19/02/2023